November 28, 2019

TANTRADE YAJIVUNIA MAFANIKIO KWA KIPINDI CHA MIAKA 4 YA RAIS MAGUFULI

 Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa  Khamis, akizungumza  na waandishi (hawapo pichani).


Na Asha Mwakyonde

MAMLAKA  ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade), katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli imeweza kupata mafanikio mbalimbali yakiwamo utoaji wa taarifa za upatakinaji wa masoko ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 27, 2019 Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis, amesema kuwa  TanTrade imekuwa na jukumu utoaji taarifa za upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi, tangu mwaka 2017 hadi 2019.

Mkurugenzi huyo amesema tayari  jumla ya Kampuni 31,891 zilishapatiwa taarifa mbalimbali za kibiashara kuhusu bei na masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi. .

"Katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano  wafanyabiashara 405 waliweza kuunganishwa na masoko na kuuza tani 102,000 za mahindi, tani 2,000 za karanga, tani 5,000 za soya, tani 50 za ufuta, tani 7 za majani ya papai, kilogramu 200 za unga wa ubuyu, tani 2 za iliki, tani 5,000 za muhogo na tani 3.2 za tangawizi ya unga., " amesema.

Ameongeza kuwa miongoni mwa bidhaa zilizoonesha uhitaji mkubwa katika masoko ya nje ni pamoja na matunda, samaki na mazao ya bahari (mwani), jamii ya mikunde, asali, kahawa, chai, korosho, viungo na vyakula.  Maulizo hayo yalitoka katika nchi za India, Nchi za ukanda wa SADC, China, Japan, nchi jirani za Afrika Mashariki (EAC), Falme za Kiarabu, Misri, Marekani, Vietnam na Ulaya.

Latifa amesema kuwa mbali na mafanikio hayo  ya kusambaza taarifa za uhitaji wa bidhaa TanTrade kwa kushirikiana na Wanunuzi kutoka nchi mbalimbali iliratibu semina za kutangaza fursa za biashara katika nchi zao ikiwa ni muendelezo wa kimkakati wa kupenya katika masoko yao.

Anesema semina mbalimbali ziliratibiwa ambapo wafanyabiashara na wadau 425 walishiriki ili kutambua fursa za masoko ya nje na taratibu za kuyafikia masoko katika nchi za Uswidi, Ufaransa, Ukraine, China na Rwanda.

" Semina hizi ni za Kutangaza fursa za Masoko zilifanyika Uswizi na  idadi ya washiriki ilikuwa 40, bidhaa  zenye fursa ni Korosho, Kahawa, Chia  na Matunda yaliyosindikwa," amesema Mkurugenzi huyo.

Ameeleza kuwa fursa nyingine zilifanyika  nchini Ufaransa ambapo  idadi  ya washiriki 20, bidhaa zenye fursa tani 1,849 za matunda, viungo, kahawa, karanga na korosho na pia Ukraine; Idadi ya washiriki 135, bidhaa zenye fursa Kahawa, Chai, viungo (mdalasini, iliki na viungo mchanganyiko) na ufuta.

Amefafanua kuwa nchini China; Idadi ya washiriki 120, bidhaa zenye fursa tani 2,000 za karanga, tani 3,000 za ufuta, tano 5,000 za maharage ya soya nazo zilipata fursa za kimasoko.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Rwanda; Idadi ya washiriki 110, bidhaa zenye fursa ya mahindi tani 102,000.

Pia Mkurugenzi huyo amezungumzia  ukuaji na uendelezaji wa Masoko ya Nje ya Nchi amesema TanTrade imeendelea kukuza na kuendeleza bidhaa za kutafuta masoko kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF).

Amesema TanTrade imeendelea kuratibu Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) kwa lengo la kutoa fursa za kutangaza bidhaa.

No comments:

Post a Comment

Pages