HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 21, 2019

Kilimo hai kinga ya magonjwa yasiyoambukiza

Baadhi ya wanahabari, wakulima kilimohai na wawezeshaji wa semina kuhusu kilimohai wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kutembelea shamba la mkulima Remmy Temba mkazi wa Shimbwe Juu, kata ya Uru Wilaya ya Moshi VijijijI mkoani Kilomanjaro.
Alama inayotumika kitambulisha bidhaa zilizolimwa kwa njia asili bila kemikali za viwandani. 
 

Na Irene Mark

SERIKALI imetenga zaidi ya Sh. Bilioni 898 kwa ajili ya bajeti ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Kwenye bajeti hiyo asilimia 40 ya fedha hizo inatumika kutibu wananchi wanaopata magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni Saratani, Kisukari, Figo, Moyo na Shinikizo la damu.

Kutengwa kwa fedha hiyo ni dalili kwamba kasi ya wagonjwa hao imeongezeka hivyo kuongeza mzigo kwa Serikali na kuyumbisha nguvu kazi ya taifa na uchumi wa kaya.

Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Magembe, amekiri kuwa fedha nyingi zinatumika kushughulikia magonjwa yasiyoambukizwa.

"Ndio maana Serikali imeona upo ulazima wa kuwa na mpango wa kushughulikia magonjwa haya kwa kuangalia upande wa matibabu na kujikita zaidi katika kuzuia watu wasiambukizwe," anasema Dk. Magembe.

Wakati Serikali ikitafuta njia za kuzuia watu wasiambukizwe, Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM), limedhamiria kurejesha uasili wa maisha ya Watanzania na kupunguza kasi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kubadili mtindo wa ulaji.

Mjumbe wa Bodi ya TOAM, Richard Mhina, anasema hivi sasa magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha hali inayowafanya watu kupoteza kabisa uasili wao.

Mhina alisema hayo hivi karibuni Mjini Moshi, Kilimanjaro wakati wa ziara ya mafunzo ya uandishi sahihi wa habari za kilimohai yaliyoandaliwa na TOAM kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Ziara hiyo ya siku tatu ilihusisha waandishi wa habari na wachora vibonzo kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambao walijifunza kwa nadharia na vitendo njia za kuandaa shamba, kupanda, kutumia mbegu na mbolea asili ili kupata chakula kisichoandaliwa kwa kutumia kemikali.

Mjumbe huyo wa Bodi alisema kwa viwango vikubwa, magonjwa yasiyoambukizwa yanatokana na ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye kemikali za viwandani alizosema kuwa ni hatari kwa afya.

Anasema vyakula vya asili ni dawa na kinga ya maradhi pia hivyo kuitaka jamii kuanza utaratibu wa kula vitu vya asili ambavyo hivi sasa vimeadimika.

"Unajua wazee wa zamani waliishi miaka mingi kwa kuwa hawakula wala kutumia vinywaji vyenye kemikali, hii iliwaweka mbali na maradhi.

"Tatizo letu ni kwamba tumeiga mtindo wa maisha ya watu wa magharibi, tunaishi maisha ya wenzetu ambayo kwa kweli yanaharibu jamii na kupoteza hata uasili wetu na mazingira pia," anasema Mhina.

Anakiri kwamba zipo changamoto kwa jamii katika kurejea kwenye uasili wake hivyo kuwataka wanahabari kupeleka taarifa sahihi kwa wananchi ili nao waone umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa lengo la kuboresha afya zao.

Muwezeshaji kwenye mafunzo hayo, Constantine Akitanda, anasema kilimohai ni fursa muhimu ya kuboresha afya na kipato kwa kuwa mazao ya asili huuzwa kwa gharama kubwa.

Akitanda ambaye pia ni mtaalam wa mawasiliano TOAM, anasema soko la dunia linahitaji zaidi vyakula vya asili ambavyo kuanzia mbegu hadi chakula hakina kemikali

"Kilimohai kumekuwepo tangu mababu na mambabu, lakini baada ya kuanza mapinduzi ya viwanda mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia, viwanda vya mbolea ya kemikali vilijengwa, hapo ndipo tulianza kuharabu mfumo wetu wa asili.

"Lakini wapo watu waliukataa mfumo wa kemikali wakaamua kuendelea na mfumo wa asili ambao leo tunauita kilimohai kilichohusisha sayansi pia," anasema Akitanda.

Akitanda anasema fursa za kilimo hai zipo huku akibainisha kwamba hadi kufika Septemba 2019 wakulima 500,000 wamesajiliwa kufanya kilimohai hapa nchini na kukamata soko la mazao hayo ndani na nje ya nchi.

"Kwenye kilimo hai kuna uwekezaj wa Dola milioni sita za Marekani Afrika na kwenye soko la Dunia kuna uwekezaji wa Dola bilioni 81," anasema Akitanda.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo wa mawasiliano, Tanzania inaongoza kwa kuwa na ardhi inayofaa kwa kilimo hai kwa lengo la kuboresha afya kwa kula chakula bora na kufanya kilimo endelevu kwa vizazi vijavyo na kulinda ikolojia kwa kulima bila kutumia mbolea za kemikali.

Anasema kwa mashamba  yaliyokuwa yakiwekewa mbolea  za kemikali yanapewa likizo ya miaka mitatu kisha kupima kiwango cha sumu katika ardhi kabla ya kuanza kilimo hai.

"Ili ufanye kilimo hai lazima kuthibitishwa na kupewa alama maalum ili uweze  kuuza mazao katika ukanda wa Afrika Mashariki kwani mazao hai huuzwa nje ya nchi kwa gharama kubwa... mfano ni kahawa inaongoza kwa bei kilo moja kwenye soko la dunia inauzwa kwa Dola 10 wakati iliyolimwa kwa mbolea za kemikali inanuniwa chini ya Dola tatu.

Anasema ili kupata soko zaidi, wanapanga kuingia kwenye zao la korosho huku akibainisha changamoto yake ni  kilimo hai  kutopendwa kwa sababu mbalimbali licha ya kuwa utafiti wa mwisho ulionesha uzalishaji ni asilimia 50 kwa kilimo hai na asilimia 50 cha kutumia dawa.

Akitanda anabainisha kwamba Bara la Afrika kuna azimio la 18 Afrika ifikapo 2025 kuhakikisha wanafikia malengo ya kuboresha afya za wananchi kwa kutumia mazao yanayotokana na kilimo hai kwa kuheshimu asili ya viumbe ili kuwa na maendeleo endelevu, kutumia njia za kubadilisha mazao shambani ili kutunza ardhi.

Anasema kilimo hai hakiruhusu kuua wadudu shambani badala yake wanatumia njia asili kuwafukuza ili kuruhusu ustawi bora wa mazao.

No comments:

Post a Comment

Pages