Kikosi cha Invicta Sauro FC kikiwa katika picha ya pamoja na kocha wao aliyetimuliwa kazi wa kwanza kushoto.
MILAN, ITALIA
HISTORIA imeandikwa, baada ya juzi Jumamosi kocha Massimiliano
Riccini kufutwa kazi nchini Italia baada ya kuiongoza timu yake Invicta Sauro
FC kushinda mabao 27-0 dhidi ya ya Marina Calcio katika Michuano ya Ligi ya
Vijana, sababu ikitajwa kuwa ni udhalilishaji.
Rais wa Invicta Sauro FC ya Grosseto mjini Tuscany,
Paolo Brogelli, amesema ushindi huo dhidi ya Marina Calcio ni wa udhalilishaji
na haukuwa na lengo la kuwafunza watoto wa timu iliyoshindwa wala iliyoshinda, hivyo
uongozi wa timu umeamua kumfuta kazi kocha huyo.
“Wapinzani wetu lazima waheshimiwe, mimi kama Rais wa
timu kuna vitu sijaviona uwanjani leo. Kufunga mabao mengi ni udhalilishaji, mbali
na mabao, nilitegemea kuona watoto wanaelimishwa zaidi uwanjani kuliko kufunga.
“Hicho kitu leo sijakiona, makocha wanatakiwa
kuwafundisha wachezaji hususani watoto wao nidhamu na kuheshimu wapinzani,” alisema
Brogelli kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.
Hii sio mara ya kwanza kocha kutimuliwa kazi
kutokana na aina hiyo ya matokeo, kwani mwaka 2015, Serranos Sub 11 ya Hispania
iliichapa Benicalap FC kwa mabao 25-0, matokeo yaliyomfukuzisha kazi kocha wa
Serranos, Pau Cercos, kwa kilichoitwa kukosea heshima timu pinzani.
No comments:
Post a Comment