Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akifundisha matumizi sahihi kunyunyuzia
dawa za kuua wadudu haribifu wa mazao jana kwa wakazi Wilayani Igunga
wakati uzinduzi wa msimu wa kilimo kwa Mkoa wa Tabora.
Na Tiganya Vincent
MKUU wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri amesitisha kwa muda likizo za Maafisa Ugani na Maafisa Kilimo wa
ngazi zote, huku akiwataka kutumia kipindi msimu wa kilimo kwenda kwa wakulima kwa
ajili ya kutoa elimu na kuwasaidia kulima kilimo bora.
Mwanri alitoa kauli hiyo jana
Wilayani Igunga wakati akizungumza na Wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo Pamba
na Maafisa Ugani kutoka Halmashauri mbalimbali alipokuwa akizindua msimu wa
kilimo kwa Mkoa wa Tabora.
Alisema kimsingi likizo
ni haki ya Mtumishi yoyote, lakini inapaswa kutoa athari shughuli za uzalishaji
kwa wakulima ambao wanategemea maelekezo kutoka kwao kwa ajili ya uzalishaji
wenye tija.
“Kipindi
hiki mvua
zimeanza kunyesha na tayari wakulima wameanza kulima …mnapaswa kwenda
kutoa
elimu kwa wakulima ili waweze kulima mazao yote kwa kufuata kanuni za
kilimo
bora…kila zao ni lazima lilimwe kwa kuzingatia vipimo na liwe katika
mstari ili
kuongeza uzalishaji...ni marufuku kwa Afisa Ugani kusafiri nje ya Kituo
chake kipindi hiki labda kwa dharura na kwa sababu ambayo iko nje ya
uwezo wa binadamu” alisema.
Alisema wakulima wasiposaidiwa
wataendelea kulima kilimo cha duni na cha kizamani ambacho wanatupa mbegu bila utaratibu
na kuwa na uzalishaji wa kujikimu badala ya kuzalisha ziada ambayo itasaidia
kujiendeleza na viwanda nchini kupata malighafi za kutosha.
Mwanri aliongeza Afisa
Ugani wakati wa masika ni sawa na alivyo Mwalimu kipindi cha masomo naye hawezi
kwenda likizo kipindi ambacho shule zinakuwa bado hazijafungwa.
Alisema mara baada ya shughuli
za kilimo kumalizika , Maafisa hao wataruhusiwa kuendelea na likizo zao za
mwaka na kuwataka Maafisa Utumishi kupanga Kalenda za likizo za watumishi hao kwa
kuzingatia kalenda ya kilimo.
No comments:
Post a Comment