November 21, 2019

Mourinho kuinoa Tottenham

JOSE Mourinho
LONDON, UINGEREZA
 
JOSE Mourinho, ametangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa Tottenham Hotspur ya London, Uingereza, huku akifichua siri ya ‘kulamba matapishi yake’ na kukubali ajira ya kuinoa Tootenham kuwa ni mipango sahihi waliyonayo.

Mourinho aliyechukua mikoba iliyoachwa wazi na kocha aliyetupiwa virago juzi Jumanne, Mauricio Pochettino, aliwahi kukaririwa mwaka 2015 akisema kuwa hawezi kamwe kuinoa Spurs katika maisha yake, kwa sababu anawapenda mashabiki wa mahasimu wao Chelsea.

Mourinho, kocha wa zamani wa Chelsea na Manchester United, amesaini kandarasi ya kuinoa Spurs hadi mwishoni mwa msimu 2022/23, huku akisema ubora wa Tottenham na kituo chao cha soka la vijana ndio kitu pekee kilichomvutia kuingia mkataba huo.

"Ubora wa vikosi vyote, ikiwa ni pamoja na timu ya vijana," alisema Mourinho juu ya kilichombadili kauli yake ya kutoinoa Tottenham, na kuongeza: "Kufanya kazi na wachezaji wa aina iliyopo Tottenham, ndicho kilichonivutia."

Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy alisema: "Katika Jose (Mourinho), maana yake nikuwa tumepata kocha mwenye mafanikio na heshima kubwa katikaa mchezo wa soka."
Levy amekubali kumlipa Mourinho mshahara wa pauni milioni 15 kwa mwaka, mara mbili ya alivyokuwa akimlipa Pochettino na kibarua cha kwanza kwa kocha mpya kitakuwa mechi ya London Derby dhidi ya mahasimu wao West Ham United, Novemba 23.

Chini ya Pochettino, Tottenham ilifuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL)  msimu uliopita, lakini ikapoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Majogoo wa Jiji Liverpool katika fainali kali mjini Madrid, Hispania.

Pochettino raia wa Argentina, ambaye aliajiriwa Tottenham Mei 2014, hajawahi kuipa timu hiyo taji lolote ikiwa chini yake, ambako ubingwa wao mwisho kwa Spurs ulikuwa ni wa Kombe la Ligi mwaka 2008.

Levy aaliongeza kuwa anaamini katika uzoefu alionao Mourinho na kwamba Mreno huyo anaweza kuwa tiba ya anguko la klabu yake kwa kuamasha ari mpya katika vyumba vya kuvalia vya timu hiyo, iliyohamia uwanja mkubwa zaidi mwaka huu.

Mourinho ni kama yuko nyumbani jijini London, ambako anakumbukwa kwa kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika miaka ya 2005, 2006 na 2015, pamoja na taji moja la FA aliyotwaa katika vipindi viwili vya kuinoa Chelsea.

Akiwa na Manchester United kuanzia Mei 2016, Mourinho anayependa kujiita ‘The Special One,’ alitwaa taji la Europa League na Carabao Cup 2017, kabla ya kutimuliwa kazi klabuni Old Trafford Desemba 2018.

BBC Sport

No comments:

Post a Comment

Pages