November 15, 2019

SBL yahimiza Usalama Barabarani Msimu wa Sikukuu

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kupambana na ajali za barabarani, hususani nyakati za Sikukuu za Mwisho wa Mwaka, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), jana imetoa vifaa mbalimbali vya usalama barabarani pamoja na elimu kwa madereva wa mabasi na waendesha bodaboda mjini Moshi.

Msaada huo ni muendelezo wa kampeni ya nchi nzima ya Kampuni ya SBL kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, hasa madereva inayojulikana kama ‘Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’ inayohamasisha madereva kuepuka kuendesha wakiwa wamekunywa kilevi.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanywa na Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL, John Wanyancha na kushuhudiwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohamed. 

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na makoti ya usalama barabarani, stika, vipeperushi vyenye ujumbe juu ya usalama barabarani, pamoja na programu za elimu zilizotolewa kupitia redio na kwenye vyuo vya elimu ya juu vilivyopo mjini Moshi.

“Tunapoelekea msimu wa Sikukuu za mwisho wa mwaka, Kampuni ya SBL inapenda kuwakumbusha wateja wake na umma kwa ujumla, kusherehekea sikukuu zinazokuja kistarabu kwa kuhakikisha hawaendeshi vyombo vya moto baada ya kutumia kilevi,” alisema Wanyancha.

Kwa upande wake, Kamanda Zauda, aliishukuru SBL kuandaa kampeni hiyo na kuongeza kuwa kwa kulishirikisha Jeshi la Polisi, kampuni hiyo inaiunga mkono Serikali katika kutoa elimu ya usalama barabarani na pia kupambana na ajali zinazosababishwa na ulevi.

Aliwaonya madereva na watumiaji wengine wa barabara wanaotumia kilevi na kuendesha vyombo vya moto  bila kufikiria athari za kufanya hivyo na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitawavumilia watu wa aina hiyo hasa katika kipindi hiki kuelekea Msimu wa Sikukuu.

“Tunapenda kuona barabara zetu zinaendelea kubaki salama kwa kipindi chote cha msimu wa sikukuu. 

“Hatupendi kuona uharibifu wa mali, majeruhi au mtu kupoteza maisha kwa sababu ya ajali zinazosababishwa na utumiaji pombe usio wa kistarabu na sababu nyinginezo,” alisema Zauda.

No comments:

Post a Comment

Pages