Na Mwandishi Wetu
KATIKA kupambana na ajali za barabarani, hususani
nyakati za Sikukuu za Mwisho wa Mwaka, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), jana
imetoa vifaa mbalimbali vya usalama barabarani pamoja na elimu kwa madereva wa
mabasi na waendesha bodaboda mjini Moshi.
Msaada huo ni muendelezo wa kampeni ya nchi nzima ya
Kampuni ya SBL kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara, hasa madereva
inayojulikana kama ‘Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’
inayohamasisha madereva kuepuka kuendesha wakiwa wamekunywa kilevi.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanywa na Mkurugenzi
wa Mahusiano kwa Umma wa SBL, John Wanyancha na kushuhudiwa na Kamanda wa Kikosi
cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohamed.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na makoti ya usalama
barabarani, stika, vipeperushi vyenye ujumbe juu ya usalama barabarani, pamoja
na programu za elimu zilizotolewa kupitia redio na kwenye vyuo vya elimu ya juu
vilivyopo mjini Moshi.
“Tunapoelekea msimu wa Sikukuu za mwisho wa mwaka, Kampuni
ya SBL inapenda kuwakumbusha wateja wake na umma kwa ujumla, kusherehekea
sikukuu zinazokuja kistarabu kwa kuhakikisha hawaendeshi vyombo vya moto baada
ya kutumia kilevi,” alisema Wanyancha.
Kwa upande wake, Kamanda Zauda, aliishukuru SBL kuandaa
kampeni hiyo na kuongeza kuwa kwa kulishirikisha Jeshi la Polisi, kampuni hiyo
inaiunga mkono Serikali katika kutoa elimu ya usalama barabarani na pia
kupambana na ajali zinazosababishwa na ulevi.
Aliwaonya madereva na watumiaji wengine wa barabara
wanaotumia kilevi na kuendesha vyombo vya moto
bila kufikiria athari za kufanya hivyo na kusisitiza kuwa Jeshi la
Polisi halitawavumilia watu wa aina hiyo hasa katika kipindi hiki kuelekea Msimu
wa Sikukuu.
“Tunapenda kuona barabara zetu zinaendelea kubaki
salama kwa kipindi chote cha msimu wa sikukuu.
“Hatupendi kuona uharibifu wa mali, majeruhi au mtu
kupoteza maisha kwa sababu ya ajali zinazosababishwa na utumiaji pombe usio wa
kistarabu na sababu nyinginezo,” alisema Zauda.
No comments:
Post a Comment