November 27, 2019

SERA MPYA YA AFYA KUJIKITA ZAIDI KWENYE KINGA

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akifungua Kongamano la 6 la mwaka la Afya lenye lengo la kuwaleta pamoja Wadau mbali mbali katika Sekta ya Afya, ili kujadili maendeleo na changamoto ambazo nchi inakabiliana nazo.


Na WAMJW- DOM

Sera Mpya ya Afya ya Mwaka  2019 - 2020 itajikita katika Kinga ili kukabiliana na mzigo wa gharama za matibabu ambazo zinawatesa Wananchi katika ngazi ya Jamii na nchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu jiji hapa wakati akifungua kongamano la 6 la mwaka la Afya lenye lengo la kuwaleta pamoja Wadau mbali mbali katika Sekta ya Afya, ili kujadili maendeleo na changamoto ambazo nchi inakabiliana nazo, lenye kauli mbiu ya "ufanisi na matokeo " katika utoaji huduma za Afya.

"Ukiangalia Sera ya Afya ya Mwaka 2007, tulijikita zaidi kwenye mambo ya Tiba, sio kinga, kwahiyo Sera hii mpya ya Afya ya mwaka 2019 - 2020 itajiwekeza zaidi katika masuala ya Kinga sio Tiba, kwa sababu wote tunaamini Kinga ni bora kuliko tiba" alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo alisema Sera hiyo inapendekeza kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Wadau iweke miundombinu ya kutoa huduma za Afya kwa kuzingatia vigezo vya jografia ya eneo husika, idadi ya watu waliopo katika eneo, na kuangalia mzigo wa magonjwa katika eneo hilo.

"Serikali kwa kushirikiana na Wadau tutaweka miundombinu ya kutoa huduma za Afya kwa kuzingatia vigezo vitatu, vigezo vya kijografia ya eneo husika, vigezo vya idadi ya watu waliopo katika eneo, na vigezo cha tatu tutaangalia mzigo wa magonjwa katika eneo hilo ili kumpatia mwananchi huduma stahiki na kwa wakati kulingana na vigezo hivi" Alisema.

Aidha , amesema Sera hiyo mpya inayotarajia kuanza kutumika mwaka huu wa fedha , Serikali itaendelea kutambua mchango wa Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi, jambo litalosaidia kupunguza mzigo wa utoaji huduma.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Kongamano la Afya Omary Nchili amesema kuwa, lengo la Mkutano huo, ni kujadili changamoto na matokeo chanya katika Sekta ya Afya, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi.

"Tumekutana hapa Wadau mbali mbali kuweza kujadili, changamoto pamoja na matokeo chanya katika Sekta ya Afya, kwa ufanisi, hivyo tutakuwa hapa kwa siku mbili ambazo tutapembua kwa undani kuhusu upatikanaji wa huduma kwa gharama ndogo na upatikanaji wa huduma kwa ujumla " alisema.

Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya Zanzibar, Tume ya huduma ya Kijamii ya Kikristo, Bakwata na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tindwa Medical Services inayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete .

No comments:

Post a Comment

Pages