Na Mwandishi Wetu-WAMJW
Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Ummy Mwalimu ametoa pole kwa Anna Zambi mwenye umri wa miaka 16,
ambaye amefiwa na wazazi wake wote wawili pamoja na ndugu zake watatu.
Waziri Ummy ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa
mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo tayari kutoa msaada wa kisaikolojia.
“Pole nyingi kwa binti yetu Anna Zambi, hili jambo
ni kubwa mno kwa huyu mtoto, inaumiza sana, ninamwombea kwa Mungu ampe nguvu na
moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,nasi Wizara tukiwa na jukumu na
dhamana ya kusimamia ustawi na maendeleo ya watoto nchini tunachukua jukumu la
kuratibu na kusimamia psychosocial support ya mtoto huyu pamoja na masuala
mengine yanayohusu ustawi wake kwa ujumal” alizema Waziri Ummy.
Waziri Ummy alimuagiza Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. John Jingu kuratibu masuala ya utoaji wa huduma ya kisaikolojia kwa
Mtoto Anna na Katibu Mkuu huyo amemtembela mtoto Anna nyumbani kwao Goba jijini
Dar es Salaam na kutoa salamu za polekwa niaba ya Wizara.
Akizungumza mara baada ya kutoa salamu za pole Dkt.
John Jingu amesema kuwa Wizara imeshatoa Maafisa wa Ustawi wa Jamii kuanza kutoa huduma ya msaada wa kisaikolojia
kwa Mtoto Anna na kuuhakikisha kuwa Serikali itamsaidia Mtoto huyo ili aweze kurudi
katika hali yake ya kawaida.
Ameongeza kuwa Serikali itakuwa bega kwa bega na familia
katika kuhakikisha mirathi inasimamiwa vizuri ili aweze kupata haki zake zote
bila kuingiliwa na mtu yoyote kwani ni yupo katika wakati mgumu sana kwa
kuondokewa na familia yake yote.
“Nikuhakikishie tutasimamia na utapata msaada
mzuri na tunaamini utakaa sawa na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuoe nguvu na
faraja katika kipindi hiki kugumu unachopitia tuko pamoja na wewe” alisema Dkt.
Jingu
Wazazi wa Anna- Lingston Zambi na Winfrida Lyimo
pamoja na ndugu zake watatu Lulu, Adrew na Grace walifariki Dunia Oktoba 26
mwaka huu wakiwa njiani kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani
Kilimanjaro, kwenye mahafali ya Kidato cha Nne ya Anna, ambapo gari waliokua
wakisafiria lilisombwa na maji na mafuriko yaliyotokea wilayani Handeni mkoani
Tanga.
No comments:
Post a Comment