Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia)
akimsikiliza Msimamizi wa ujenzi wa mradi wa maji mji wa Magu, Mhandisi Wilbert
Bujiku akielezea hatua zilizofikiwa za ujenzi wake.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia)
akitoa maelekezo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji
Magu.
Na Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Mhandisi Anthony Sanga ametoa muda wa siku 14 kwa Mkandarasi China Civil
Engineering Construction Corporation (CCECC) kukamilisha ujenzi wa mradi wa
maji Mji wa Magu.
Ametoa agizo hilo Novemba 22, 2019
alipofanya ziara kwenye mradi huo Wilayani Magu, Mkoani Mwanza ili kujionea
hatua ya ujenzi iliyofikiwa sambamba na kuzungumza na Mkandarasi.
Mara baada ya kutembelea eneo la
chanzo cha maji na kituo cha tiba ya maji cha mradi, Mhandisi Sanga alibainisha
kuwa ameridhishwa na ujenzi wa mradi na kwamba tayari wananchi wameanza kupata
huduma ya maji lakini yapo maeneo machache ambayo bado hayajakamilika
inavyopasa na hivyo kumtaka Mkandarasi kuhakikisha anayakamilisha kwa muda
aliyopangiwa.
“Mradi unaridhisha umejengwa vizuri
ila tu shida ninayoiona hapa kuna maeneo machache bado hayajakamilishwa vizuri
ambayo kitaalam tunaita 'snags' kama kuna pipe imechomoka, koki, kurudishia
rangi, na vingine vidogo vidogo. Maelekezo yangu ni kwamba ndani ya
wiki mbili kuanzia leo maeneo haya yakamilike,” alisisitiza Mhandisi Sanga.
Aliongeza kuwa Mkandarasi
amekwishafanya kazi kubwa na kwamba hizo chache zilizobaki ahakikishe
anazikamilisha haraka na kwamba baada ya siku hizo 14 awe amekabidhi mradi kwa
Mamlaka ya Maji Mji wa Magu na awe ameondoka kwenye eneo la mradi ili
kuondokana na gharama mbalimbali za usimamizi wake.
“Hata kama hatumlipi mkandarasi kwa
hizi kazi zilizobakia lakini gharama bado zitakuwepo tu ikiwa ni pamoja na
kulipa watendaji wetu ambao ni wasimamizi wa mradi fedha za kujikimu na gharama
zingine zikiwemo za usafiri wa kuja kukagua kazi mara kwa mara na hivyo kutumia
mafuta,” alisema Mhandisi Sanga.
Aliongeza kuwa fedha za ujenzi wa
mradi ni za wananchi kwani zilitolewa na wadau wa maendeleo ambao aliwataja
kuwa ni Benki ya Maendeleo ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kama
mkopo wa masharti nafuu ambao Serikali inapaswa kulipa.
Alitahadharisha kwamba Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Dk. John Pombe Magufuli haipo tayari kushuhudia
matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na kwamba haitowavumilia wakandarasi
wanaochelewesha miradi kote nchini bila sababu za msingi.
“Namshukuru sana Mhe. Rais ambaye
kimsingi ndio mtoaji wa fedha, tunasema fedha imetolewa na wafadhili lakini ni
mkopo wa masharti nafuu na hivyo zitalipwa kwa kodi za wananchi, kwa hiyo
tutahakikisha hata shilingi ya mwisho inatumika vizuri na hatuwezi kumtazama
Mkandarasi afanye anavyojisikia yeye wakati wa kukamilisha mradi,” alisema
Mhandisi Sanga.
Akizungumzia maeneo ambayo
hayajafikiwa na mradi na uhitaji upo, Mhandisi Sanga alielekeza Mamlaka ya Maji
Mwanza (MWAUWASA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Magu (MAUWASA) pamoja na
Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wayafanyie kazi na kwamba kwa maeneo
yatakayokuwa nje ya uwezo wao wayawasilishe wizarani ili wananchi wote
waliokusudiwa waweze kunufaika na mradi huo.
Aidha, alishukuru uongozi wa Mkoa wa
Mwanza na Wilaya ya Magu kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Magu, kwa ufuatiliaji
na usimamizi mzuri wa mradi na kwa uhamasishaji walioufanya kwa wananchi
waliokuwa wakidai fidia.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la
Magu, Boniventura Kiswaga aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa
mradi huo mkubwa wa maji ambao aliuelezea kuwa ni mwarobaini wa kero ya muda
mrefu ya upatikanajni wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wake.
Naye msimamizi wa mradi kutoka
MWAUWASA, Mhandisi Wilbert Bujiku aliahidi kusimamia vyema utekelezaji wa
maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu na kwa wakati kama ilivyoelekezwa.
Aidha, akiwasilisha taarifa ya mradi
kwa ujumla, Mhandisi Bujiku alisema mradi utanufaisha zaidi ya wananchi 120,000
na kwamba hadi hivi sasa jumla ya kaya 4,911 tayari zimeunganishwa na wanapata
huduma ya maji na kwamba vituo 21 vya kuchotea maji pia vimejengwa maeneo
mbalimbali kulingana na idadi ya wakazi wa maeneo husika.
Aliongeza kuwa mradi umehusisha
ujenzi wa tenki la lita milioni mbili za maji, ulazaji wa bomba kuu kutoka
ziwani hadi kwenye tenki umbali wa kilomita 10.9 na bomba za usambazaji kwa
wananchi umbali wa kilomita 67 na kwamba umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni
16.
No comments:
Post a Comment