Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati), akielekeza jambo
wakati wa ziara ya kukagua athari ya mvua kwenye miundombinu ya maji Wilayani
Handeni. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe na kulia ni Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo.
Na Mwandishi Wetu
Serikali
imewahakikishia wakazi wa Handeni, Mkoani Tanga uendelevu wa huduma ya maji
licha ya kuharibika kwa miundombinu ya maji kulikosababishwa na mvua
zinazoendelea kunyesha.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa kauli hiyo hapo
juzi wilayani hapa wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua athari ya mvua
kwenye miundombinu ya maji sambamba na kupata ufumbuzi wa haraka kufuatia hali
ya mvua zilizonyesha kwa takribani wiki mbili mfululizo.
Mara
baada ya kujionea hali halisi, Mhandisi Sanga aliwatoa hofu wananchi wa Handeni
ambapo aliwataka kuwa watulivu na aliahidi kuwa Serikali itahakikisha huduma ya
maji inarejea haraka iwezekanavyo.
"Ninawasihi
wananchi kufanya subira na kuwa watulivu na kuzingatia maelekezo ya
Serikali," alisisitiza Naibu Katibu Mkuu Sanga.
Mhandisi
Sanga alibainisha kuwa zoezi la tathmini ya athari ya mvua hizo kwenye
miundombinu ya maji wanaloendelea nalo halitochukua zaidi ya siku tatu kama
ilivyoagizwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.
"Waziri
wa Maji ametuagiza kuharakisha kukamilisha zoezi hili, nasi tutahakikisha
linafanyika kwa kasi ikiwa ni pamoja na kutazama njia mbadala ili wananchi
wapate huduma ya maji kwa haraka," alisema Mhandisi Sanga.
Aliongeza
kuwa Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli haipo tayari kuona wananchi wake
wanataabika na kwamba hatua madhubuti na za haraka zinachukuliwa ili
kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Awali
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela akielezea kwa ujumla athari za mvua hizo
kwenye Mkoa wa Tanga, alisema kuwa zimeleta madhara kwenye miundombinu ya
barabara na madaraja na kusababisha huduma ya usafiri katika maeneo mbalimbali
kuathirika.
“Tulichokibaini
katika mvua hizi zilizonyesha ni kuwa zimeharibu mabwawa ya maji na kusababisha
maji yaliyotoka katika mabwawa hayo kuathiri miundondombinu mbalimbali ikiwemo
ya maji na barabara,” alieleza Shigela.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akielezea athari za mvua
hizo alisema ni pamoja na kuharibika kwa mabwawa 11 ya maji yanayotumiwa na
wakazi wa Handeni na maeneo jirani na kati ya hayo yapo mabwawa makubwa matano
ambayo aliyataja kuwa ni Kwenkambara, Mandera, Suwa, Msomera na Mkomba.
Aidha,
Gondwe alipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe
Magufuli kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa wakati na kwa hatua
mbalimbali za haraka zinazoendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kurejesha
mawasiliano ya miundombinu ya barabara na maji iliyoathirika.
Sambamba
na hilo, Gondwe alimpongeza Mhandisi Sanga na timu ya wataalam aliyoambatana
nayo kutoka Wizara ya Maji na taasisi zake kwa kufika Wilayani hapa mapema ili
kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya mabwawa ya maji ili kupata
ufumbuzi.
“Kwa
niaba ya wananchi wa Wilaya ya Handeni tunatoa shukrani nyingi sana kwa
Mheshimiwa Rais kwa kutujali na kuwatuma watendaji wa Serikali kufika hapa
Handeni ili kutatua matatizo yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha,”
alisema Gondwe.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mhandisi
Clement Kivegalo ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Sanga alisema kuwa
wanaendelea na tathmini ila kwa mabwawa yaliyopasuka wamebaini yalijengwa chini
ya kiwango na pia hayakuwa yakitunzwa inavyostahili na hivyo kupelekea
kuharibika wakati mvua hizo zilizonyesha.
No comments:
Post a Comment