November 14, 2019

TASAF yatumia Bil.2/- kuboresha elimu, afya

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Alvera Ndabagoyo akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari na maofisa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), waliotembelea ofisini kwake Novemba 13, 2019.


Na Irene Mark, Arusha

ZAIDI ya Sh. Bilioni mbili zimetumika kuboresha miundombinu ya elimu na afya kwenye vijiji 45 vya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha jijini Arusha ambavyo vimefikiwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Maboresho hayo yamefanyika baada ya vikao vya wanavijiji kuibua kero zinazoeakabili katika maeneo yao ambapo jumla ya miradi 44 imetekelezwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Alvera Ndabagoye, alisema mbali na fedha hizo TASAF imetoa ruzuku ya Sh. Bilioni 7.2 kwa kaya 9,107 za wananchi maskini zaidi kwenye halmashauri hiyo.

Alisema mwaka 2014/2015 baada ya TASAF kuingia wilayani humo na kuanza utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini, kata 21 zenye vijiji 45 na kaya 9,107 zimefikiwa na mradi huo.

"Miradi iliyotekelezwa imegusa sekta ya elimu na afya kwa kuboresha na kujenga madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, mabweni, samani na Ujenzi wa nyumba za walimu.

"...Kwa sekta ya afya TASAF imetusaidia kujenga Zahanati kwenye kata ya Midawe na mpaka sasa ujenzi unaendelea," alisema Ndabagoye.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, TASAF imefany miradi ya kuongeza kipato kwa walengwa ambayo ni ufugaji wa mbuzi wa maziwa, kuku wa asili na kilimo cha mbogamboga.

"Tunawashukuru sana TASAF katika utekelezaji wa shughuli zake kwa wananchi wetu wanatoa pia ajira za muda na wanaoshiriki wanalipwa ili waendelee kujipatia kipato na kujikimu.

"Katika eneo hilo, shughuli zinazofanyika ni utunzaji wa mazingira, ukarabati wa barabara na mifereji ya umwagiliaji," alisisitiza Ndabagoye.

No comments:

Post a Comment

Pages