November 14, 2019

Wanasayansi wataka uwekezaji kwenye utafiti

Dk. Amos Nungu
Na Suleiman Msuya 
WANASAYANSI kutoka nchi 15 za Kusini mwa Jangwa la Sahara, taasisi na nchi rafiki duniani wameshauri Serikali mbalimbali kuongeza uwekezaji katika shughuli za utafiti na ubunifu ili kutatua changamoto kwenye jamii.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolijia (COSTECH), Dk. Amos Nungu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano  huo wa Baraza la Sayansi Kanda ya Afrika unamalizika leo jijini Dar es Salaam.
Alisema mkutano huo mkuu wa mwaka ambao umeshirikisha wajumbe zaidi ya 250 umekuwa wa mafanikio makubwa kwa wajumbe kusisitiza uwekezaji kwenye eneo la utafiti na ubunifu kama chachu ya nchi maskini kupiga hatua za maendeleo.
Dk. Nungu alisema awali walianza kujadili na kuangalia  mifumo katika uwekezaji wa mifumo ya utafiti na ubunifu ili kutoa matokeo chanya kwa wananchi na nchi zao.
“Niseme mkutano huu mkuu wa mwaka umekuwa na mafanikio makubnwa sana kwa washiriki hasa Tanzania kama muandaaji kwani mjadala ulilenga tunachokisimamia,” alisema.
Alisema wajumbe walishauri utafiti ufanyike kwa mahitaji ya nchi husika na sio kufuata matakwa ya wafadhili jambo ambalo Tanzania wanalitekeleza kwa asilimia kubwa.
Mkurugenzi huyo wa COSTECH alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya utafiti na ubunifu hivyo tume itahakikisha utafiti unaofanyika unakuwa na matokeo chanya yaonekane.
“Mwananchi wa kawaida anatakiwa kuona malengo ya utafiti un aofanyika na ili kuona matokeo ni lazima kuzingatia misingi ya utafiti hasa katika eneo la sayansi wazi,” alisema.
Aidha, alisema katika kuhakikisha utafiti unaofanyika unakuwa na tija wamekuwa wakishirikisha nchi zilizoendelea ili kuona kama zinakuwa na uwiano.
Dk. Nungu alisema iwapo utafiti utakuwa wa wazi na shirikishi utasaidia watafiti hasa wa nchi jirani kushirikiana kwa kupeana taarifa bila kufichana.
Alisema pia watafiti wanapaswa kushirikiana hasa katika eneo la miundombinu kama maabara ambazo kwa nchi za Afrika hazipo.
Dk. Nungu alisema iwapo utafiti unaofanywa na watafiti watapewa kipaumbele ni wazi kuwa maendeleo ya nchi husika yatapatikana.

No comments:

Post a Comment

Pages