November 27, 2019

USHIRIKIANO WATAKIWA KUKABILI RUSHWA YA NGONO

 Ofisa Mwandamizi wa Utawala na Masuala ya Jinsia kutoka Uboalozi wa Ireland, Aran Corrigan, akitoa hotuba yake wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yalifanyika leo jijini Dar es Salaam.
 Agnes Hanti kutoka UN Women Tanzania, akizungumza katika maadhimisho hayo. 


Na Suleiman Msuya

JAMII imetakiwa kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini hasa vitendo vya rushwa ya ngono ambavyo vimekithiri.

Hayo yamesemwa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Watoto na Wazee, Beatrice Mgumiro, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yalifanyika leo jijini Dar es Salaam.

Alisema takwimu zinaonesha unyanyasaji wa kijinsia upo nchini kwa asilimia 28 hivyo jitihada za pamoja ndio zinaweza kumaliza changamoto hiyo.

Mgumiro alisema maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu ya "Kataa Rushwa ya Ngoni Jenga Kizazi Chenye Usawa' hivyo ili kutafsiri kaulimbiu hiyo kivitendo ni lazima ushirikiano wa pamoja uwepo.

Alisema Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), Mtandao wa Kupambana na Kuzuia Rushwa ya Ngono, Jeshi la Polisi taasisi nyingine wameonesha nia ya   kukabiliana na ukatili wa kijinsia zinapaswa kuungwa mkono.

Ofisa huyo alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wengine amewashauri wanawake kujishughulisha  na shughuli za uzalishaji na kuacha kurahisisha mambo.

"Lazima wanawake tupambane, tutoke na ulimwengu ujue mwanamke yupo na anafanya nini tuache kusubiria  kuletewa wanawake tunaweza," alisema.

Mkurugenzi wa WFT, Mary Rusimbi alisema wanashirikiana na mashirika na mitandao zaidi ya 100 ambapo katika mwaka huu watajikita katika kupinga rushwa ya ngono.

Alisema ili kukabiliana na rushwa ya ngono wamejikita kutoa elimu zaidi kwa kushirikiana na wadau wengine.

Alisema asilimia 28 ya matukio ya ukatili wa jinsia sio kiwango kizuri kwa nchi hivyo kuzitaka taasisi zote zenye uwezo wa kupambana na hali hiyo kushiriki kikamilifu.

"Kampeni hii ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia itaweza kubadilisha jamii kwa kuwa na mwitikio  mzuri wakutoa taarifa za matukio hayo ," alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania  (TUKTA) Rehema Ludanga alisema wao kama wafanyakazi wanataka ukatili wa kijinsia kufikia kikomo ifikapo 2030.

Alisema wamekuwa wakipata malalamiko ya kuwepo matukio ya ukatili wa kijinsia na kuyafanyia kazi lakini bado hali sio nzuri.

Alisema pia wamekuwa wakitoa elimu kwa wanachama wao ili waweze kutoa taarifa kwa wakati pale wanapokutana na ukatili wa kijinsia hasa rushwa ya ngono.

Alisema wakati umefika wakufanya utafiti kuhusu rushwa ya ngono pekee  ili kujua ukubwa wa tatizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Intelijensia kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Emmanuel Kiyabo aliwataka wanawake kuacha kushusha thamani yao kwa rushwa ya ngono.

Alisema ofisi yao ipo wazi wakati wowote kupokea taarifa ya matukio hayo ili wafanyie kazi.

Jaji Mstaafu Eusebia Munuo na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Janeth Magoni walisema misimamo na kujitambua ndio njia itakayomaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini.

Kwa upande wao Ofisa Mwandamizi wa Utawala na Masuala ya Jinsia kutoka Uboalozi wa Ireland, Aran Corrigan na Mwakilishi wa Ubalozi wa Canada, Pamela O'Donnell walisema tatizo la ukatili wa kijinsia lipo duniani kote hivyo kinachohitajika ni elimu na ushirikiano wa wadau wote ili waweze kutokomeza.

Wawakilishi hao wa Balozi walisema iwapo jamii itapata elimu kuanzia ngazi ya familia itasaidia kukabiliana na hali hiyo jambo ambalo kwa nchi zao linafanyika.

No comments:

Post a Comment

Pages