Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa uzio kwenye Kituo cha Afya Daraja Mbili jijini Arusha, Ibrahim Selemani akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliotembelea kituo hicho kilichojengewa uzio kwa ufadhili wa TASAF.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Daraja Mbili, Luciana Kazimoto (mwenye miwani), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu uzio uliojengwa kuzunguka kituo hicho. Kushoto ni Ofisa Muuguzi Perice Chibago.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Zuhura Mdungi (aliyeshika kinasa sauti), akifanya mahojiano na Ofisa Muuguzi wa Kituo cha Afya Daraja Mbili, Perice Chibago kuhusu hali ya utoaji huduma kabla na baada ya uzio huo kujengwa. (Picha na Irene Mark).
Na Irene Mark
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), umeongeza hadhi na kuondoa udhalilishaji uliokuwa ukifanywa kwa wajawazito na wagonjwa wanaotibiwa kwenye Kituo cha Afya Daraja Mbili jijini Arusha kwa kujenga uzio.
Uzio huo umejengwa kwa gharama ya Sh. Milioni 54 baada ya kuibuliwa kwenye kikao cha wananchi kuwa kero kubwa kwao wakati wa kikao cha mtaa na maofisa wa TASAF.
Hayo yalibainishwa na watumishi wa hospitali hiyo mbele ya wanahabari waliotembelea kituo hicho cha afya wakiongozana na maofisa wa mfuko huo kukagua miradi yenye mafanikio inayotekelezwa na TASAF.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Daraja Mbili, Luciana Kazimoto alisema kabla ya uzio huo umeondoa tatizo la wizi wa vifaa, udhalilishaji wa wagonjwa, mifugo na walevi.
"Mazingira ya kazi yalikuwa magumu ilikuwa kila wiki lazima tukute koki za mabomba zimeibwa, ndoo za maji, taa, mitungi ya gesi na vifaa vingine vya kusaidia huduma," alisema mganga huyo.
Ofisa Muuguzi wa Kituo cha Afya Daraja Mbili, Perice Chibago, alisema utoaji wa huduma kabla ya uzio ulikuwa changamoto kwa kuwa hapakuwa na faragha.
"Ilikuwa kawaida upo chumba cha kuzalisha una msaidia mama kuzaa ghafla anaingia mtu anaulizia msalani au anamtafuta mtu.
"...Wakati mwingine upo ndani unatoa huduma anaingia mlevi anaulizia msalani, kweli ilikuwa inatukwaza hapakuwa na utaratibu wa siri kwenye utoaji wa huduma kama inavyotakiwa kisheria," alisema Chibango.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa uzio huo, Ibrahim Selemani alisema ujenzi huo ulikuwa shirikishi kati ya TASAF kwa asilimia 90 na wananchi kwa asilimia 10.
"Kabla ya ujenzi changamoto ilikuwa mipaka jambo lililochelewesha kuanza kazi na tulipoanza tuliifanya kwa miezi mitatu mfululizo.
"Wakazi hasa wa mtaa wetu wa Alinyanya wamefurahi maana hata wao maeneo yao yamekuwa salama pia... polisi nao wamepungukiwa kero maana walikuwa wanakuja hapa kituoni wanawakamata mpaka wagonjwa wakihisi kuwa wezi," alisema Selemani.
No comments:
Post a Comment