November 17, 2019

ZHANG AFURAHIA KUOA TANZANIA

Na Tatu Mohamed

MWANAFUNZI wa Chuo cha Mzumbe ambaye ni raia kutoka China Jianpo Zhang amesema anajisikia fahari kuoa Tanzania akidai kufanya hivyo mbali na kudumisha undugu baina ya familia hizo pia kunazidi kuboresha Uhusiano wa nchi za Tanzania na China.

Katika kuthibitisha kwa vitendo furaha aliyonayo Raia huyo wa China amefanya sherehe kubwa ya kuwashukuru Watanzania na hasa wote ambao wameshiriki kikamilifu katika kufanikisha ndoa yake na mkewe Shamsa Shaban Zhang.

Ndoa hiyo ilifungwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa Majeshi mstaafu Robert Mboma.

Akizungumza wakati akitoa shukrani hizo Zhang amesema anajivunia kuoa mtanzania huyo akisisitiza kuwa binadamu wote ni ndugu na kitendo chake cha kufunga ndoa hiyo kitazidi kumfanya ajisikie kuwa kama yupo nyumbani huku akiwataka watanzania kuona fahari pia kwenda kuoa raia kutoka China.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu aliyoishi nchini ameona mambo mengi mazuri na  kiasi cha kumfanya ajihisi yupo ‘nyumbani’  na zaidi akidai kuwa amani na upendo kutoka kwa watanzania ndiyo hasa jambo linalozidi kumuongezea hamasa ya kuona undugu unazidi kukua baina ya mataifa yote mawili.

Ameongeza kuwa furaha kwake Tanzania inazidi kukua kimaendeleo siku hadi siku chini ya uongozi wa Rais John Magufuli  ambaye pia anasema katika utawala wake ameona wazi wazi ushirikiano baina ya Tanzania na China ukizidi kuhimarika.

“Naipenda Tanzania, nawapenda watu wake na zaidi Rais John Magufuli ambaye katika utawala wake naona mambo mengi mazuri ukiwemo ujenzi wa miradi mbalimbali ikifanyika katika kiwango cha hali ya juu” amesema Zhang.

 Amesema mipango yake ya baadae ni kufanya biashara mbalimbali zinazoakisi mahitaji  muhimu ya kijamii ili ziweze kuzidi kumuweka karibu na watanzania anaodai kuwa kwa sasa ni ndugu zake hasa baada ya kumuoa Shamsa.

No comments:

Post a Comment

Pages