Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mizengo Pinda
amewasisitiza watumishi mkoani Rukwa kuhakikisha kila mmoja katika nafasi yake anafanya
kazi kwa uadilifu na kueleza kuwa utendaji kazi wa aina hiyo ndio
njia pekee ya kupeleka maendeleo ya mkoa mbele na hatimae kuutoa mkoa
katika umasikini.
Amesema kuwa amesikitishwa na
taarifa iliyolewa hivi karibuni kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2018
ambapo mkoa wa rukwa umeonekana kushika mkia kwa kuwa na asilimia 45 ya
umasikini nchini kwa mahitaji ya msingi huku mkoa wa Dar es Salaam ukiwa na asilimia
8 ya kiwango hicho huku mkoa wa Katavi uliozaliwa kutoka mkoa wa rukwa ukiwa na
asilimia 29
Pia ameshtushwa kuwa mkoa wa
Rukwa ambao ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula
nchini kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu pamoja na kuongoza kuwa na kiwango
kikubwa cha umasikini wa chakula kwa asilimia 19 wakati Katavi ukiwa na
asilimia 9.
“Tukikaa sisi kama wataalamu,
najua baadhi ya wilaya wameshapata maafisa lishe, tutawatengenezea mfumo
tuwaonganishe na majukumu ya zahanati na vituo vya afya na hospitali zetu za
wilaya, mama anapokuwa ametunga mimba lazima aambiwe aende kliniki, lakini
kliniki si kupima tu uzito nakadhalika, hapana, kubwa ni kuona kwamba huyu mama
mzazi anapata lishe stahiki?” Alihoji.
Amesema kuwa fikra zilizopo
katika makabila yaliyopo mkoa wa Rukwa na Katavi wanaamini kuwa kula mboga za
majani ni umasikini wa kutupwa kwahiyo kama mkoa una kazi kubwa ya kubadili
fikra za watu hao na kuonyesha umuhimu wa kula mboga za majani.
Ameyasema hayo katika salamu
zake kwa watumishi wa mkoa wa Rukwa hivi karibuni ambapo kikao hicho
kiliwajumuisha wakuu wa taasisi, idara, wakala za serikali pamoja na watumishi
wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim
Wangabo.
Wakati akimkaribisha Waziri
Mkuu Mstaafu, Mh. Joachim Wangabo alimpongeza Mh. Pinda kwa kuhakikisha
anasogeza huduma muhimu kwa wananchi kwa kuugawa mkoa wa Rukwa na kuzaliwa Mkoa
wa Katavi ambapo hivi sasa wananchi wa mkoa wa Katavi wanafaidika na maendeleo
yanayopatikana kutokana na uwepo wa huduma muhimu za kijamii katika halmashauri
tano za mkoa huo.
“ Wilaya ya Mpanda ilikuwa
inapakana na Kaliua, Uvinza na inapakana na Sikonge Mkoa wa Tabora, Sasa
fikiria huyo RC aliyekuwa anatoka Sumbawanga kwenda mpaka huko, huenda ukakaa
miaka mitano usifike maeneo mingine, ilikuwa ni shida kweli na miundombinu yake
ilikuwa ni matatizo makubwa sana kwahiyo kuugawa huu mkoa wa Rukwa kuwa mikoa
miwili umetoa unafuu mkubwa sana wa kimaendeleo” Alisema.
Mkoa wa Rukwa
ulianzishwa mwaka 1974 kwa kumega sehemu ya Mikoa ya Tabora na Mbeya. Mkoa una
eneo la kilomita za mraba 27,765, kati
ya hizo Kilomita za mraba 22,844 (82.3%) ni za nchi kavu
na Kilomita za mraba 4,921 (17.7%) ni za maji. Mkoa
una jumla ya Wilaya tatu (3), zenye Halmashauri nne (4), Tarafa 16, Kata 97,
Vijiji 339, Vitongoji 1,825, Mitaa 167 na Kaya 199,766. Mwaka 2010 mkoa
uligawanywa na kuzaliwa mkoa wa Katavi.
No comments:
Post a Comment