December 20, 2019

AFISA LHRC AHOJIWA POLISI

Na Mwandishi Wetu

Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamshikilia Afisa wa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (pichani).

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwaambia waandishi wa habari leo Desemba 20, 2019, kwamba Magoti alikamatwa na wenzake watatu kutokana na makosa ya jinai.

Mambosasa hakueleza kwa kina juu ya kukamatwa na Magoti, awali taarifa zilisema Magoti alitekwa saa nne asubuhi jijini Dar es Salaam na watu ambao hawajajulikana baada ya watu hao kumkamata kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari lao aina ya Harrier, kisha wakaondoka naye kuelekea kusikojulikana.

Baada ya taarifa hizo kusambaa katika mitandao ya kijamii, Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga, alisema kwamba kabla Magoti hajatekwa, alishuka kwenye bodaboda aliyokuwa amepanda, maeneo ya Mwenge Kituo cha Mafuta cha Puma.

“Kwa mujibu wa mtu aliyetupatia taarifa, ni kwamba Magoti alipotelemka kwenye bodaboda, ghafla lilikuja gari hilo ambalo hata namba zake za usajili hazikufahamika mara moja na kuondoka naye.

“Kwa hiyo, hadi sasa tunaendelea kufuatilia juu ya tukio hilo ili tujue chanzo cha kutekwa huko na mwenzetu amepelekwa wapi,” alisema Henga.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa  Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, alisema wanasikitishwa na kutekwa kwa mwanasheria huyo ambaye ni mfanyakazi wa LHRC.

Alisema Afisa huyo ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu, alichukuliwa kwa nguvu na watu wanaokisiwa kuwa ni watano, akiwa maeneo ya Mwenge katika Kituo cha Mafuta cha Puma.

“Tukio hili lilitokea asubuhi leo ambapo watu hao walitumia nguvu kumuingiza Magoti kwenye gari aina ya Harrier wakiwa wamevalia mavazi ya kiraia.

“Lakini, jitihada za kumtafuta ndugu Tito, zinaendelea ili tujue ametekwa na kupelekwa wapi.

“Kwa ujumla, mtandao wetu unasikitishwa na kuendelea kwa matukio hayo ya utekaji kwani yameanza tena kushamiri hasa kwa watetezi wa haki za binadamu,” alisema Ole Ngurumwa.

Katika hatua nyingine, Ole Ngurumwa alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kuchukua hatua za haraka na za makusudi kuhakaikisha mtetezi huyo wa haki za binadamu anapatikana akiwa salama.

Pia, alisema watetezi wa haki za binadamu, wanahabari na wananchi kwa ujumla, wanatakiwa kuungana kwa kupaza sauti kwa ajili ya Magoti ili aweze kupatikana akiwa salama.

No comments:

Post a Comment

Pages