December 24, 2019

AFISA WA LHRC AFIKISHWA MAHAKAMANI LEO

Afisa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti,  (wa pili kushoto), akiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Desemba 24, 2019 ambapo amesomewa mashitaka matatu yakiwepo utakatishaji fedha na kuendesha programu mahususi kwa ajili ya kutenda uhalifu. (Picha na Azam Media).

Afisa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti, na mwenzake ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Tehama, Theodory Gyan, wakitoka mahakamani baada ya kuahirishwa kwa kesi inayowakabili. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na Mwandishi Wetu

OFISA Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Tehama, Theodory Gyan (36), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh. Milioni 17.

Magoti na mwenzake wamefikishwa leo Desemba 24, 2019 katika mahakamani hiyo na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega  na wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Renatus  Mkude.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Simon alidai  kuwa washtakiwa hao wawili katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya Kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh. 17,354,535.

Katika shtaka la pili, Wakili Nchimbi alidai katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi, 2019 na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji na mkoa  wa Dar es Salaam kwa pamoja washtakiwa hao na mengine ambao hawapo mahakamani walimiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa ya jinsi.

Naye Wakili Mkude alidai katika shtaka la tatu, Inadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, mwaka huu, ndani ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walijipatia jumla ya Sh. 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na madharia ya kosa la kushiriki genge la uhalifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote  kwakuwa Mahakama hiyo aina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi mpaka ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mshataka nchini (DPP).

Upande mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2019 itakapotajwa. Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili kutokuwa na dhamana.

No comments:

Post a Comment

Pages