HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 17, 2019

Benki ya NMB yatambuliwa kuwa mwajiri aliyeidhinishwa na Chama cha Wahasibu ulimwenguni (ACCA)

Benki ya NMB imepokea kibali cha ithibati kuwa mwajiri aliyeidhinishwa  na Chama cha Wahasibu cha Kimataifa Association of Chartered Certified Accountants (ACCA)  katika kutoa maendeleo stahiki ya  taaluma kwa wafanyakazi.
Utambuzi huu unamaanisha kwamba Benki ya NMB ina kiwango cha kimataifa cha kutoa fursa za wafanyakazi kujiendeleza kitaaluma na kuamini kuwa mafunzo hayo  husaidia wanachama wa ACCA kwenye benki na taaluma nyingine kukidhi mahitaji yao ya uzoefu wa vitendo makazini.
NMB walipokea utambuzi huo kutoka ACCA mwishoni wa mwaka huu, ambapo NMB inakuwa miongoni mwa taasisi 13 nchini na taasisi za kimataifa zisizopungua 7,000 duniani zinazotambuliwa na ACCA.
NMB na ACCA zitaendelea kuhakikisha wafanyakazi wanakuzwa kwa viwango vya juu zaidi. Ambapo NMB itaendeleza kuweka mazingira  mazuri na rafikii ya kufanya kazi ili kusaidia wanachama na  wanafunzi wa mafunzo ya ACCA kupata mafunzo stahiki.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Meneja  mwandamizi Idara ya Ukaguzi wa ndani NMB, Gaudence Nganyagwa, amesema ni wakati sasa wa Tanzania na Ulimwengu kufahamu jinsi gani NMB inathamini wafanyakazi wake kwa kuwajengea uwezo ili kuwa wenye ushindani katika kutoa huduma bora yenye weledi wa kimataifa.
“Tunaamini kuwa ni wakati wa kuifanya Tanzania na Ulimwengu ujue ni kwa kiasi gani NMB tunathamini maendeleo ya wafanyakazi wetu. Kwa miaka mingi, benki imekuwa ikiwekeza katika mafunzo na kuwaendeleza wafanyakazi ili kuzalisha kilicho bora sokoni.
“Tunaamini kwamba kwa ACCA kutupatia tuzo hii, imethamini na kutambua juhudi zetu za kujitolea katika kuwajengea uwezo wafanyakazi. Tunaamini kuwa kama viongozi katika tasnia ya huduma za kifedha, ni jukumu letu kuhamasisha taasisi zingine kuwekeza katika stadi za watu.”amesema Nganyagwa.
Nae Mkaguzi  wa Ndani wa NMB Sulemani Manyiwa amesema faida kubwa kwa NMB kuwa mwanachama wa ACCA ni kuifanya NMB kuwa na mwonekano wa kimataifa.
“Kuwa mwajiri aliyeidhinishwa wa ACCA kunaboresha mwonekano wa benki  kimataifa. Ni rahisi kwa NMB kuajiri na kuendeleza vipaji bora katika soko. NMB sasa inaweza kutangaza nafasi mbalimbali kimataifa  kupitia tovuti za kazi za ACCA na kushiriki katika maonesho ya kazi kimataifa.
“Hii pia itafungua milango hata kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi au wageni wanaotaka kuendeleza kazi zao na mwajiri aliyejitolea nchini Tanzania. Tafiti zetu na dodoso sasa zitashughulikiwa na ACCA ili kuongeza ufahamu wa kitaalam kwa mustakabali wa tasnia. Pia tutapigwa msasa wa mara kwa mara na mwelekeo wa tasnia na  kufanya tafiti na matukio ya pamoja na ACCA.”amesema.
Akithibitisha kuwa nafasi ya kujiendeleza kielimu na kitaaluma kwa wafanyakazi wa NMB ni ajenda nyeti na ya kimkakati, Kaimu Ofisa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Emmanuel Akonaay aliongeza kuwa uwekezaji wa benki katika kuendeleza wafanyakazi ni uwekezaji makini ambao utahakikisha benki ya NMB inaendelea kuwa benki bora katika kuvutia vipaji na kuviendeleza.
“Benki pia itapata huduma bora zaidi na za haraka kutoka kwa ofisi ya ACCA ya Tanzania kuhusu suala lolote. Wanachama waliohitimu mafunzo ya ACCA ambao ni wafanyakazi wa NMB watakuwa na uhakika wa kutunza uanachama wao, na wataweza kujiendeleza na fursa mbalimbali za ACCA katika gharama ndogo zaidi” amesema.
ACCA inafanya kazi katika nchi 179 ikiwa na  dhamira ya kuwa kiongozi wa ulimwengu katika kuunda na kuimarisha uwezo na utendaji wa uhasibu kote ulimwenguni.

No comments:

Post a Comment

Pages