December 05, 2019

CSOs zataka jamii ielimishwe kuhusu MTAKUWWA


 Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwajina Lipinga (kulia), akizungumza kwenye mjadala wa tathmini ya Mpango wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF), Anna Kulaya na Mratibu wa MTAKUWWA ofisi ya Waziri Mkuu, Happiness Mugyabuso. (Na Mpiga Picha Wetu).



 
NA MWANDISHI WETU

ASASI sizizo za kiserikali (CSOs) zimependekeza jitihada zifanyike kuelimisha umma kuhusu Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kurahisisha utekelezaji wake.

Ushauri huo ulitolewa kwenye kongamano la siku mbili kutathmini mpango huo, lilioandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF) na kushirikisha asasi binafsi na maofisa kutoka wizara mbalimbali.

Jackline Mollel kutoka TANLAP alisema bado watu wengi hawajaufahamu kuhusu mpango huo hivyo wadau wa asasi zisizo za kiserikali wanapaswa kuongeza nguvu kuelimisha umma.

“Unajua kuna watu wanatekeleza MTAKUWWA bila kufahamu sasa hawa wakielimisha kwamba huu ni mpango wa serikali watafanya zaidi kwasababu watakuwa wanajua kwamba wanaisaidia serikali,” alisema Jackline.

Rose Sarwatt kutoka asasi ya wajane ya TAWIA alisema ili mpango huo upate mafanikio makubwa lazima elimu itolewe kwa watanzania wengi ili washiriki kwenye kuutekeleza.

Alisema ingawa mwongozo umeshatolewa kuhusu halmashauri kuanzisha kamati za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto halmashauri nyingi hazijaanzisha hali inayoonyesha kuwa kuna mwamko mdogo.

Alisema changamoto kubwa kwenye utekelezaji wa MTAKUWWA ni watu kutofahamu mpango huo hivyo ni jukumu la CSOs kwenda maeneo yote ya nchi kuelimisha na kuhamasisha kuundwa kwa kamati hizo.

“Mwitikio kwenye halmashauri nyingi ni mzuri ila wengi hawajapanga bajeti kwasababu hawajaona umuhimu wa kufanya hivyo. Tunapasa kuwafuata na kuwaeleza umuhimu wa kufanya hivyo,” alisema

Ester Mongi kutoka World Vision alisema lengo la MTAKUWWA ni kuunda kamati za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto lakini anshangaa haijatengwa bajeti kwaajili ya kufanikisha mpango huo.

Alisema serikali haijafanya vya kutosha kwenye uundwaji wa kamati hizo kwani nyingi zimetengenezwa na na asasi zisizo za kiserikali ambazo uendeshaji wake mwisho wa siku utakuwa wa kusua sua.

“Hizi asasi zisizo za kiserikali nyingi ziko kwaajili ya kutekeleza miradi ya muda mfupi sasa mradi ukiisha baadhi wanaweza wasiendelee sasa hapo hizo kamati haziwezi kuwa endelevu. Serikali ilipaswa kutenga bajeti ya kuendesha kamati hizi,” alisema

Alisema kamati zinazoundwa zinapaswa kuanzia kwenye vijiji na mitaa kwani huko ndiko matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yanafanyika badala ya kuanzia kwenye wilaya na mikoa.

“Kamati zikiwa chini kabisa kuanzia kwenye kijiji halafu zikawezeshwa zikawa na nguvu sasa zikiwa na nguvu zitasaidia sana kupunguza matatizo haya yanayozidi kuongezeka kwa wanawake na watoto,” alisema.


Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Emmanuel Burton, alisema madawati ya kushughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia yanapaswa kujengwa nje ya vituo vya polisi ili kuweka hali ya usiri na uwazi kwa mtu anayekwenda kutoa taarifa za kunyanyaswa kijinsia.

Burton alisema mwongozo uliotolewa na serikali unataka madawati yote yawe nje ya vituo vya polisi ili kuwapa uhuru na usiri watu wote wanaokwenda kupata huduma za kisheria wanaponyanyaswa kijinsia.

Alisema changamoto ya fedha ndiyo imesababidha baadhi ya madawati kuwa ndani ya vituo vya polisi hali inayowanyima haki watu kwenda kutoa taarifa za unyanyazaji wa kijinsia wakiwemo wanaume.

“Mtu hawezi kwenda kwenye kituo cha polisi pale mapokezi akasema nimebakwa naomba msaada hivyo lazima kuwa na usiri ndiyo maana mwongozo unataka hivyo, lakini kama dawati liko ndani ya kituo cha polisi lazima kuwe na chumba maalum cha kazi hiyo,” alisema.

Alisema hivi sasa kuna vituo 426 vya madawati ya jinsia ambavyo vimejengwa nje ya vituo vya polisi ambavyo vinawawezesha wanaotendewa vitendo hivyo kuwa wazi na huru kutoa taarifa na kusaidiwa.
mwisho

No comments:

Post a Comment

Pages