Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony
Mavunde akihutubia vijana wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya Mkopo wa Shilingi
Milioni 92 kwa vikundi vya Vijana Wilayani Chato. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu (KAZI,
VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU).
Na Mwandishi Wetu
Serikali kufanyia maboresho
kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo zitakazomwezesha kijana mmoja mmoja
kupata fursa ya mkopo utakaowasaidia kuazisha ama kuendeleza miradi mbalimbali itakayowakwamua
kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira
Mhe. Anthony Mavunde wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya Shilingi Milioni 92
iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Mavunde alieleza
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali
ya kuwawezesha vijana kiuchumi ili waweze kuanzisha au kuendeleza shughuli za
uzalishajimali, hivyo ilianzisha kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa
vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa lengo la kutoa mikopo
yenye riba nafuu.
“Serikali kwa kuzingatia
matatizo yanayowakabili vijana wake iliona vema kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana ambao madhumini yake makubwa ni kuwapatia vijana mikopo yenye masharti
nafuu itakayowasaidia kuanzisha au kuimarisha miradi yao,” alisema Mavunde
Aliongeza kuwa, kwa
kulitambua hilo Serikali imeamua kuangalia utaratibu mzuri utakaokuwa unatoa
fursa ya kuwezesha vijana kupata mikopo hiyo, ikiwemo suala la kumwezesha
kijana mmoja mmoja kuwa na nafasi ya kupata mikopo hiyo.
“Mfano kijana akiwa ana
mradi wake na akawa na vigezo vya kukopesheka ni vyema akapatiwa mkopo ili
aweze kujiendeleza kiuchumi kwa kuwa atakuwa na uwezo wa kuzalisha ajira kwa
vijana wengine,” alisema Mavunde
Alieleza kuwa hapo awali lengo
la kutoa mkopo huo kwa vikundi vya vijana ilikuwa ni kuwezesha vijana
kuendeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji mali wanayoifanya pamoja na kuinua
kipato chao na hatimae waweze kujikwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa Ofisi ya
Waziri Mkuu katika kulisimamia hilo imekuwa ikiendeleza ukuaji wa ujuzi wa
vijana hao kwa kuanzisha Mpango wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi
wa biashara ili kabla ya kupatiwa mikopo waweze kuwa na ujuzi utakaowasaidia kuimarisha
na kusimamia biashara zao kwa weledi na kuwa na mbinu za kukuza biashara zao.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde
amewataka vijana kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kutumia maarifa
waliyonayo kubuni miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ili waweze kukua
kiuchumi.
“Nipongeze vikundi vya
vijana vipatatavyo 12 kutoka wilaya ya Chato, Geita na Bukombe vilivyopatiwa
Mkopo, hatua mliyofikia itachangia kwa kiasi kikubwa uanzishwaji wa viwanda
vidogo vidogo vya ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kuongeza ukuaji wa
uchumi,” alieleza Mavunde
Kwa upande wake Mbunge wa
Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Kalemani ameeleza kuwa jumla
ya vikundi 783 vimeweza kusajiliwa katika mkoa wa Geita na baadhi ya vikundi hivyo
vipo vya vijana wa wilaya chato ambavyo vimenufaika na mkopo huo uliowasaidia vijana
kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi ikiwemo ufugaji, kilimo, uchimbaji
wa madini, uvuvi na biashara.
“Tunaipongeza sana Serikali
kwa kutoa fursa ya mitaji kwa vijana ili waweze kuendeleza miradi ya vikundi
vyao ambavyo vitachochea ukuaji wa uchumi wa chato,” alisema Kalemani
Sambamba na hayo Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu alieleza kuwa katika
mkakati wa programu ya kukuza ujuzi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni
vyema ikiwawezesha vijana kupata stadi za kazi katika utoaji huduma katika
mahoteli ili kuendeleza na kukuza sekta ya utalii.
“Uwepo wa hifadhi ya Burigi
Chato imekuwa ni kichocheo cha ukuaji wa sekta ya utalii katika kanda ya ziwa, itakuwa
vizuri nguvukazi ya vijana ikapata ujuzi stahiki utakaowawezesha kujua taratibu
za uendeshaji wa sekta hivyo ambayo imekuwa ni kivutio kwa wageni wa nje,”
alisema Kanyasu
Naye Mmoja wa vijana
walionufaika na mkopo huo Bw. Leonard Ngaza ameishukuru Serikali kwa kuwapatia
mkopo huo ambao utawasaidia kundeleza shughuli walizokusudia ili waweze
kurejesha kwa wakati.
No comments:
Post a Comment