December 03, 2019

KESI 391 ZA RUSHWA YA NGONO ZARIPOTIWA TAKUKURU


 Afisa wa Takukuru Mkoa wa Kagera, John Joseph, akitoa elimu kwa waandishi wa habari juu ya madhara yatokanoyo na rushwa ya ngono.
 Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki semina ya TAKUKURU juu ya kupinga vitendo vya rushwa ya ngono hapa nchini.


Na Alodia Dominick, Bukoba

Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera amesema, kwa mwaka 2017 vitendo vya rushwa ya ngono vilivyoripotiwa hapa nchini ni kesi 391.

Afisa huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, John Joseph, ametaja takwimu hizo leo wakati akitoa semina kwa waandishi wa habari mkoani humo juu ya madhara yatokanayo na rushwa ya ngono hapa nchini ambapo ameeleza kuwa, kwa mwaka 2017 kesi zilizoripotiwa za kuombwa rushwa ya ngono kwa wanawake ni 391 na kesi zilizofanyiwa uchunguzi ni 46.

Ameongeza kuwa, vitendo vya kuomba rushwa vipo ingawa bado wanaofanyiwa vitendo hivyo hawajahamasika kuviripoti kwa TAKUKURU ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na kuwa katika mkoa wa Kagera ni watu wawili tu waliotoa taarifa.

Ametaja  lengo la mafunzo hayo kuwa ni kutaka kuelimisha jamii ili watu wakemee vitendo hivyo na wavunje ukimya pia Takukuru inataka iwajengee watu kujiamini.

Pia amesema, wataanzisha dawati la kukemea rushwa ya ngono na wanategemea kufanya utafiti katika vyuo.

Hata hivyo, amesema Taasisi hiyo imeanzisha kampein ya utatu, lengo kupambana na rushwa ya barabarani ambayo inatajwa kwa kiasi kikubwa kusababisha ajali za barabarani.

No comments:

Post a Comment

Pages