December 03, 2019

MAJALIWA AAGIZA UJENZI WA MACHINJIO UKAMILIKE MWEZI HUU MWISHONI KAMA ILIVYOAMRIWA NA RAIS MAGUFULI

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati akiwasili kwenye Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa, Vingunguti jijini Dar es Salaam, Desemba 3, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mshauri wa Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Vingunguti, Henry Mwoleka, wakati alipokagua mradi huo, Desemba 3, 2019, jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa, yaliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Vingunguti, Mhandisi Elisante Ulomi, wakati alipokagua mradi huo, Desemba 3, 2019, jijini Dar es Salaam.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Afisa Mfawidhi wa Machinjio Vingunguti, Jihadhari Mgeni, wakati alipokagua machinjio hayo, Desemba 3, 2019, jijini Dar es Salaam.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akioneshwa jambo na Afisa Mfawidhi wa Machinjio Vingunguti, Jihadhari Mgeni, wakati alipokagua machinjio hayo, Desemba 3, 2019, jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kukagua Machinjio ya zamani yaliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam, baada ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Vingunguti, Desemba 3, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kukagua Machinjio ya zamani yaliyopo Vingunguti jijini Dar es Salaam, baada ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Vingunguti, Desemba 3, 2019.


Na Mwandishi Wetu


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka mkandarasi anayejenga machinjio ya kisasa ya Vingunguti jijini Dar es Salaam ahakikishe kwamba anakamilisha ujenzi huo mwishoni mwa mwezi huu kama alivyoamriwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo leo (Jumanne, Desemba 3, 2019), Mheshimiwa Majaliwa amesema amefurahishwa na hatua ya mkandarasi huyo ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ya kuongeza idadi ya watalaam na mafundi ili kuhakikisha kwamba kazi hiyo inafanyika haraka na kukamilika kwa wakati ulioamriwa na Rais Magufuli yaani Desemba 30, mwaka huu.

Amesema amefurahi pia kuona kwamba mkandarasi huyo ameamua kufanya kazi usiku na mchana, hatua ambayo imeongeza kasi ya ujenzi huo na anaamini kuwa kazi hiyo itakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Majaliwa amemtaka  Mshauri Mwelekezi wa mradi huo ambaye ni M/SCONS AFRIKA LIMITED na FB Consultant wa Dar es Salaam  asimamamie kwa karibu ili  kujiridhisha  kuwa maelekezo yote yaliyopo kwenye michoro ya ujenzi huo yanazingatiwa na mkandarasi.

Amesema Serikali imeamua kujenga machinjio hayo ya kisasa ya Vingunguti baada ya kugundua kwamba wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake  katika machinjio hayo, walikuwa wakifanya kazi zao kwenye mazingira duni na  kwamba nyama iliyokuwa ikitoka kwenye machinjio hayo ilikuwa haikubaliki kwenye soko la nje ya nchi.

“Uamuazi wa Serikali kujenga machinjio haya, utaifanya nyama inayotoka hapa ikubalike kwenye masoko ya nje ya nchi, hatua ambayo itaongeza mzunguko wa fedha kwenye eneo hili wakati Serikali na Manispaa watanufaika kwani kutakuwa na ongezeko la makusanyo ya kodi,” aliongeza Mheshimiwa Majaliwa.

Waziri Mkuu pia ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Manispaa ya Ilala wafanye mazungumzo na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili ijengwe reli ya mchepuko kutoka reli ya kati kwenda kwenye machinjio ya Vingunguti ili mifugo iingizwe moja kwa moja kwenye machinjio hayo badala ya kuteremshiwa Pugu halafu ikapelekwa  kwa magari.

Amewahakikishia wafanyabiashara wote wanaoendesha shughuli zao kwenye machinjio hayo kuwa ujenzi wa machinjio ya kisasa  ya Vingunguti hautawafanya wapoteze fusa zao za biashara au kuajiriwa kwenye eneo hilo kwani  machinjio hayo yatafungua fursa zaidi za biashara na ajira kwao.

Amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala wahakikishe kwamba wanaushirikisha uongozi wa wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake wa Vingunguti ili wanachama wao wenye sifa za kuajiriwa, waajiriwe na pia wawaandalie mazingira ya kufanya biashara mbalimbali karibu na machinjio hayo.

Akizungumzia soko na bei duni ya ngozi za mifugo nchini, Waziri Mkuu amekemea tabia ya wafugaji ya kuweka alama kwenye ngozi za mifugo yao hasa ng’ombe kwani kufanya hivyo kunashusha thamani ya ngozi za Tanzania na badala yake amewataka waweke alama za hereni kwenye masikio ya mifugo yao ili kulinda ubora wa ngozi za mifugo yao.

Amesema Serikali tayari imekwishampata mwekezaji kutoka Misri ambaye amekubali kuwekeza kwenye kiwanda cha ngozi cha Mwanza hatua ambayo italihakikishia Taifa soko la ngozi.

Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri amesema ujenzi wa machinjio hayo ulianza Julai 8, mwaka huu na mkandarasi alitakiwa akamilishe ujenzi huo ifikapo  Januari 6, 2021. Amesema kufuatia agizo la Rais Magufuli alilolitoa Septemba 16, mwaka huu, ujenzi huo unatakiwa ukamilike ndani ya miezi mitatu yaani ifikapo Desemba 31, 2019.

Bw. Shauri amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo itagharimu sh.  12, 498,916,063.00 ambapo sh. 8,528,486,470.00 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu na sh. 3, 970,429,593.00 zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na kwamba ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 60.

Akisoma risala  ya Ushirika wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake  wa Vingunguti (UWAMIVI), Mwenyekiti wao, Bw. Joel Meshaki aliiomba Serikali  iwaandalie wafanyabiashara hao eneo mbadala la kufanyia shughuli zao  ili  ajira yao isipotee.

Alipendekeza kwa Waziri Mkuu maeneo matatu yaliyoko karibu  eneo hilo, ambayo yangewafaa wafanyabiashara hao wakati watakapoondoka  kwenye maeneo yao sasa yanapojengwa machinjio ya kisasa kuwa ni Dampo la zamani ambalo kwa sasa halitumiki,  eneo la Wizara ya Kilimo ambalo kwa sasa ni sehemu ndogo tu inayotumika  na jengo la Kilimo ambalo kwa sasa linatumika kama ghala.

Alisema idadi ya mifugo inayochinjwa katika machinjio hayo kwa sasa ni ng’ombe 550 hadi 600 kwa siku za kawaida na siku za sikukuu ni ng’ombe 1,000 hadi 1,500. “Halmashauri yetu ya Ilala  hukusanya  zaidi ya sh.  milioni 118 kwa mwezi  wakati Serikali Kuu hukusanya milioni 117 kila mwezi,” alisema Meshaki.
 

No comments:

Post a Comment

Pages