December 12, 2019

KIGOMA WAHIMIZWA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA

MKOA wa Kigoma umetajwa kuwa na kiwango cha juu ya asilimia 61 ya ukatili wa kijinsia, vitendo vinavyofifisha maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Hali hiyo imetajwa kuchangiwa maradufu na jamii kutokwenda kutoa ushahidi mahakamani, punde wahalifu wanapotiwa mbaroni na mamlaka za Polisi.

Hayo yameelezwa na Shirika linalopinga ukatili dhidi ya wanawake na wasichana la Kivulini, wakati wa mdaharo wa kuadhimisha Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, uliofanyika Kijiji cha Kasanda, Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma.

Afisa Miradi wa Kivulini, Eunic Mayengela, amesema kiwango hicho cha ukatili lazima kidhibitiwe hadi kufikia ziro, mapambano yanayotakiwa kuimarishwa zaidi na jamii yenyewe.

"Mfano tu, juzi mtoto mdogo wa miaka saba ameripotiwa kubakwa na kijana wa miaka 27. Tena amekuja kugundulika siku zimepita baada ya kufanyiwa ukatili huo.

"Hebu fikiria mtoto mdogo huyu ameingiliwa kingono madhara yake ni makubwa kiasi gani? Unakuta mwanamke anapigwa na kupata ulemavu wa maisha. Tunasema hapana sasa," amesema.

Afisa huyo wa Shirika la Kivulini amesema ukatili wa kimwili unaendana na vipigo, ukatili wa kiuchumi, kingono na kisaikolojia vinaharibu maendeleo ya jamii na taifa zima, hivyo ukomeshwe.

Ametolea wito Watanzania wakiwamo wana Kigoma na Kakonko, kujitokeza mahakamani kwenda kutoa ushahidi dhidi ya wahalifu wa masuala ya ukatili.

"Ukiwa wewe ndiye umefanyiwa ukatili wa aina yoyote, kupigwa, kubakwa, kunyimwa fursa za kufanya biashara, kutukanwa matusi ya nguoni, kubakwa au kulawitiwa, toa taarifa polisi.

"Kesi nyingi zinakwama mahakamani kwa sababu ya kukosa ushahidi. Mwananchi yeyote una wajibu kwenda kutoa mahakamani ili aliyefanya ukatili aweze kufungwa na hatimaye kukomesha hii hali," Mayengela amesisitiza.

                       POLISI

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kakonko, S.F. Njau, kupitia taarifa yake iliyosomwa na Askari wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani hapa, Getruda Bahisha, amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2019, kesi 313 za ukatili wa kijinsia zikiwamo za kingono zimeripotiwa.

Kulingana na SP Njau, matukio mengi ya vitendo hivyo ni shambulio, ambapo pamoja na mambo mengine zaidi ya wanafunzi 2,000 wa shule mbalimbali wilayani hapa, wamepatiwa elimu ya kupiga vita ukatili huo.

"Matukio ya kubaka, mwaka 2016 kesi 11, mwaka 2017 matukio 16, mwaka 2018 matukio 19 na mwaka huu zimeripotiwa kesi tisa," amesema Afande Getruda wakati akisoma taarifa hiyo ya OCD Njau.

Amesema kesi 41 zimekwama mahakamani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kukosekana ushahidi, huku kesi 97 watuhumiwa wake wakihukumiwa
kwenda jela gerezani.

                MKUU WA WILAYA

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hoseah Ndagala, pamoja na kuagiza vyombo vya dola kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahalifu wa masuala ya ukatili, ametaka kuongezwa zaidi elimu kwa jamii.

Amesema elimu zaidi inahitajika katika kukabiliana na vitendo vya ukatili, kwa mashirika, Serikali na wadau wa maendeleo vikiwamo vyombo vya habari kushirikiana kuleta usawa wa kijinsia.

Amesema chanzo kikuu cha ukatili wa kijinsia ni umasikini kwa jamii, hivyo alihimiza watu kufanyakazi kwa jitihada ili kujinasua na utegemezi kiuchumi.

"Lakini, ninyi wanawake ni chanzo mojawapo. Mnasema nitumie hela na ya kutolea. Ooh mara bodaboda, chipsi, mara unanunuliwa simu mimba hiyo.

"Ninyi ni hazina ya taifa. Kataeni na muwe mstari wa mbele kupinga unyanyaswaji na utegemezi. Watu wafanyekazi," amesema Mkuu huyo wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Ndagala.

Pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa Ulinzi na Usalama wilayani hapa, amesisitiza umuhimu wa waathiriwa wa ukatili, jamii na majirani wa watu wanaotendewa unyama huo kwenda mahakamani kutoa ushahidi.

  WANANCHI

Jakline Petro, mkazi wa Kakonko mkoani hapa ameeleza kuwa wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia, jambo linalowaumiza katika nafsi na kuwanyima jitihada za kimaendeleo.

Amesema manyanyaso wanayoyapata yanawanyima amani, hivyo kuomba polisi watendaji kuwakamata wanaume wanaofanya vitendo hivyo na kuwafikisha mahakamani.

"Wanawake nao wanawatendea ukatili watoto wadogo. Wanawatuma sokoni kwenda kuuza vitumbua na vibalagala," amesema Emmanuel Makoko, mkazi wa Wilaya ya Kakonko.

Kauli hiyo iliwaibua wanafunzi waliokuwa mdaharoni hapo, ambapo wameeleza kuwa baba ndiyo wanawaowatuma kwenda sokoni kuuza vitumbua, huku wengine wakisema ni mama zao huwapa amri hiyo.

 Ya 1-2 Afisa wa Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma, Getruda Bahisha, akisoma taarifa ya Mkuu wa Polisi, S.F. Njau, kuhusu vitendo vya ukatili wilayani humo.
 Baadhi ya mabango yaliyokuwa na waandamanaji, huku watoto wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hoseah Ndagala.

No comments:

Post a Comment

Pages