December 11, 2019

Waandishi wa habari watakiwa kushiriki katika shindano la uandishi wa makala

Na Janeth Jovin

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limewataka waandishi wa habari na wanafunzi waliopo vyuoni wanaosomea fani ya uandishi wa habari  kujitokeza kwa wingi kushiriki shindano la uandishi wa makala linaloendeshwa na Shirika hilo.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Kaimu Posta Master Mkuu wa Shirika hilo Mwanaisha Said wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu Umoja wa Posta Afrika (PAPU) uasisiwe mwaka 1980.

Said anasema katika kuadhimisha miaka hiyo 40 tangu kuanzishwa kwa umoja huo wameamua kuleta shindano hilo kwa waandishi wa habari na wanafunzi waliopo vyuoni ili waweze kuandika makala zinakazoisaidi jamii kuelewe kwa undani shughuli zinazofanywa na zinazoendelea kufanywa na Shirika la Posta.

Anasema makala hizo zitakazoandikwa zinatakiwa kuwa na maneno kati ya 1000 hadi 2000 huku mwandishi akitakuwa pia kuonesha anwani yake sahihi ikiwa na email, namba ya simu pamoja na jinsi yake.

"Andika makala ukielezea umuhimu wa anwani za makazi na misimbo ya Posta (Postcode) katika kujenga Tanzania ya viwanda, unaweza kuandika kwa kiswahili au kiingereza, shindano hili linaanza rasmi leo (jana) na litamalizika Desemba 31 mwaka huu.

Makala zitakazoandikwa zitumwe kwa njia ya EMS kwa anuani ya Meneja Masoko wa Shirika hili la posta mtaa wa Ghana, sanduku la posta 9551, 11300 Dar es Salaam, " anasema Said.

Anasema shindano hilo litapelekea kuchaguliwa kwa washindi 10 ambao makala zao zitakuwa bora zaidi, hivyo watapata zawadi mbalimbali zikiwemo kompyuta mpakato, simu tanashati, digito kamera, vyeti na fedha taslimu.

"Washindi watatu wa awali watakabidhiwa zawadi zao na mgeni rasmi ambaye ni Rais John Magufuli siku ya kilele cha maadhimisho ya sherehe hiyo itakayofanyika Arusha Januari 18, 2020, makala bora kabisa ya mshindi wa kwanza itasomwa mbele ya mgeni rasmi siku hiyo na makala zote tatu sasa zitachapishwa kwenye moja ya magazeti yanayochapishwa kila siku hapa nchini," anasema.

Said amewataka waandishi sasa hasa wale wa makala kuchukua fursa hiyo kuonyesha umahiri wao mbele ya Rais na wawakilishi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa Umoja huo barani Afrika ambao watahudhuria maadhimisho hayo.

"Kwetu hili ni shindano la kwanza kuwashirikisha waandishi wa habari, tutaendelea kuwashirikisha mara kwa mara katika mashindano haya, nia ni kuendeleza ushirikiano wetu mzuri wa muda mrefu na waandishi ambao kwetu sisi nyie ni wadau muhimu wa maendeleo ya sekta nzima ya posta," anasema.

Aidha anasema mbali na changamoto mbalimbali walizonazo, kwa miaka ya hivi karibuni Shirika hilo limeweza kujizatiti na kupata faida hivyo kuweza kutoa gawio kwa serikali mara mbili ambapo mwaka 2016/17 walitoa Sh. Milioni 250 na mwaka 2017/18 walitoa milioni 350.

Kwa upande wake Meneja Mkuu Menejimenti ya Rasilimali za Shirika hilo, Macrice Mbodo anasema maadhimisho hayo yamelenga kuwaleta nchi wanachama wa umoja huo wa posta kutafakari pamoja na kutambua mchango wa Mwalimu Nyerere aliyekuwa na wazo wa kuweka Shirika hilo la posta.

No comments:

Post a Comment

Pages