December 23, 2019

MBUNGE KUANZISHA MIKOPO YA ZANA ZA KILIMO

Lydia Lugakila, Kagera

Mbunge wa jimbo la Bukoba vijijini Mkoani Kagera Mhe, Jason Samsoni Rweikiza (pichani) ameahidi kuanzisha Mikopo mbalimbali ya zana za kilimo kwa wakulima mkoani Kagera ikiwemo Matrekta, na mbegu za mikopo ili kuongeza ufanisi unaolenga kuachana na jembe la mkono kwa wakulima hao.

Mhe, Samsoni Rweikiza ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia fursa ya uwepo wa kiwanda cha kusindika Nyanya  Victoria Edibles kulichopo mkoani Kagera kinacholenga kuwanufaisha wananchi waishio Mkoani Kagera na nje ya mkoa huo pamoja na Watanzania kwa ujumla.

Mhe, Rweikiza amesema kuwa katika hali ya kuhakikisha sekta ya Kilimo inaongezewa ufanisi atahakikisha huduma bora inatolewa kwa wakulima mkoani humo ikiwemo kuwapatia wakulima Matrekta ya kulimia kwa mkopo lengo likiwa ni kuachana na jembe la mkono, kukopeshwa mbegu maalum zitakazoagizwa toka mkoani Arusha.

Amesema wakulima hao watanufaika na ukopeshwaji wa mbolea, Mashine za umwagiliaji Maji, madawa ya kilimo cha Nyanya ili wananchi wazalishe kwa wingi ili kupata pesa ya kutosha.

Ameongeza kuwa huduma hizo za mkopo kwa wakulima hao zitasaidia kuongeza mapato yenye tija na faida kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Aidha ameongeza kuwa katika kuitikia wito wa Rais Magufuli atahakikisha mitambo ya kupakia maji, mitambo ya kusaga maparachichi na maembe inaletwa mkoani Kagera ili kulima katika viwango vyenye kuleta tija.

Hata hivyo amewataka wananchi mkoani humo kuchangamkia  fursa ya uwepo wa Kiwanda cha kusindika nyanya ili kujikwamua ki uchumi.

No comments:

Post a Comment

Pages