December 23, 2019

Simba Jamii kutangaza utaliii


Na Suleiman Msuya

KUNDI la wanachama na washabiki Timu ya Simba maarufu ‘Simba Jamii’ limejipanga kufanya ziara ya kutembelea vivutio vya utalii na kuvitangaza nchini na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa jana na Katibu wa Kundi hilo, Severine Kasimba "Chelsimba" wakati akizungumza na gazeti jijini Dar es Salaam.

Kasimba alisema ‘Simba Jamii’ imepania kufanya kazi ya kuielimisha jamii ya Tanzania kupenda na kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza mapato kwa Serikali.

“Simba Jamii tumekuwa tukihamasisha mambo yanayohusu timu yetu na tumefanikiwa kuwapa wafuasi wengi, ila kwa sasa tunajipanga kuelekezanguvu zetu kwenye kutangaza vivutio vya utalii na mapema mwakani tunatarajia kwenda Hifadhi ya Taifa Saadan,” alisema.

Alisema kundi hilo chini ya Mwenyekiti, Gabriel Ntole "Meneja Kijana" litatumia wanakundi wake kuhakikisha sekta ya utalii inatangazwa.

Kasimba alisema iwapo wao wakishirikiana na sekta nyingine ni sekta ya utalii inaweza kupaa na kuongeza mapato mengi na kuchochea maendeleo.

Alisema Hifadhi ya Taifa ya  Saadani iliyopo Bagamoyo ni sehemu pekee duniani ambayo ipo pembezoni mwa bahari.

Katibu huyo alisema mkakati mwingine wa ‘Simba Jamii’ ni kutangaza hifadhi mpya ya Burigi iliyopo Kanda ya Ziwa.

“Kwa sasa wakati tukipanga taratibu za kuanza ziara hizo za kuitangaza na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kutembelea hifadhi zetu ili kuwa mabalozi, pia tupo  mbioni katika kuhimiza wanamichezo wote kushirikiana nao na kuukuza utalii kwa kupitia sekta ya michezo,” alisema.


No comments:

Post a Comment

Pages