Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Dkt Angeline Mabula akizungumza na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipokutana kwa lengo la kuboresha
utendaji kazi wa Shirika hilo. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkurugenzi Mkuu wa
NHC Dkt Maulid Banyani.
Na Munir Shemweta, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekutana na Menejimenti ya
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa saa nne na kulitaka shirika hilo
kuhakikisha kufikia Januari 2020 inawachukulia hatua wapangaji wote wa Shirika
hilo wanaodaiwa kodi inayofikia bilioni 8.23.
Dkt Mabula alikutana na
Menejiment ya Shirika hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam ikiwa ni
mkakati wake wa kulifanya Shirika la Nyumba la Taifa kuimarika kimapato pamoja
na kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Alisema, katika kuifanya NHC
inaimarika kimapato ni lazima madeni kutoka kwa wapangaji wake yanakusanywa kwa
kuanzisha opreresheni maalum inatakayowezesha kutambuliwa wadaiwa wote wa kodi ili
waweze kulipa kwa wakati.
‘’Ukiacha zile taasisi za
serikali, wote wanaodaiwa ikifika januari 2020 wafikishwe kwenye vyombo vya
sheria na zile taasisi za serikali mkamuone Katibu Mkuu HAZINA ili taasisi hizo
zikatwe fedha moja kwa moja’’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakati wa zoezi la kufanya
opresheni ya kukusanya madeni sheria lazima ifuatwe ikiwemo kutoa hati za wito
wa madai kwa wadaiwa wote kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Umiliki na Uendelezaji wa Shirika la Nyumba la Taifa Greyson Godfrey
alimueleza Dkt Mabula kuwa, pamoja na NHC kuimarika katika makusanyo lakini liko
kwenye mikakati maalum wa kukusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wake na moja ya
jitihada zake ni kuingia makubaliano maalum ya namna wadaiwa watakavyolipa
madeni.
Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulid Banyani alisema Shirika lake limekuwa na
mikakati mbalimbali ya kuhakikisha linaimarika kimapato ikiwemo kutoa motisha
kwa watumishi wanaofanya vizuri katika mikoa itakayofikia lengo la makusanyo
na kutokuwa na malimbikizo ya madeni
kutoka kwa wadaiwa wa kodi.
‘’Tumekuwa tukitoa
motisha kwa watumishi wanaofanya vizuri na sasa tunaangalia ile mikao ambayo
haina malimbikizo ya madeni kwa wapangaji wake kwa asilimia mia moja tuone
namna tutakavyotoa motisha ili kuhamasisha mikoa kutokuwa na madeni’’
alisema Dkt Banyani
Aidha,
Dkt Banyani alisema,
kwa sasa NHC imeanza kufanya uhakiki kwa wapangaji wake ili kubaini
wapangaji waliopangisha watu wengine ambapo eneo la Ubungo limetumika
kama eneo la majaribio na
tayari wapangaji sita washaondolewa na kusisitiza kuwa zoezi hilo
litakuwa ni
la nchi nzima.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mabula aliagiza kupatiwa orodha ya nyumba zote za NHC zilizouzwa, zisizouzwa, zilizopangishwa
na zisizozopangishwa, viwanja vya Shirika hilo visivyoendelezwa pamoja na Nyumba zilizokuwa za Msajili
wa Majumba zilizohamishiwa NHC hilo ili kujua hali ya shirika na
mkakati wake katika kuleta ufanisi.
Pia
Dkt Mabula alitembelea maendeleo ya ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti
na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ambao uko katika hatua za
mwisho za kukamilika.
No comments:
Post a Comment