Na Veronica Mwafisi,
MOHA-Dar es Salaam
UHUISHAJI takwimu za
wakimbizi waishio jijini Dar es Salaam na mikoa mingine nchini, unapaswa
kufanywa kwa umakini mkubwa kwani unagusa usalama wa nchi.
Mkurugenzi Msaidizi
wa Uendeshaji Makambi na Makazi, kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara
ya Huduma kwa Wakimbizi, Nsato Marijani, aliyasema hayo jana wakati akifungua
mafunzo ya uhuishaji takwimu za wakimbizi.
Mafunzo hayo
yalifanyika kwenye Ukumbi wa Polisi Officer’s Mess, Oysterbay, Dar es Salaam
yakihusisha watendaji wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi, Uhamiaji, Ofisi ya Rais,
Polisi pamoja na UNHCR.
Alisema uhuishaji takwimu
utahusisha wakimbizi wote waishio jijini Dar es Salaam wenye nyaraka, walioruhusiwa
kuishi nje ya kambi za wakimbizi, maeneo mengine kuanzia kesho (Novemba 4), saa
2 asubuhi hadi Novemba 7, mwaka huu.
Alifafanua kuwa,
uhuishaji huo utafanyika katika Ofisi za Shirika la Relief of Development
Society (REDOSO), zilizopo eneo la Biafra, Kinondoni.
“Matarajio ni
kuhuisha takwimu za wakimbizi 243 lakini idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana
na wakimbizi kutoka nchi mbalimbali ambao watajitokeza.
Marijani alisema
idara zote ambazo zinahusika na uhuishaji takwimu hizo, zinapaswa kufanya
uhakiki huo kwa umakini mkubwa kwani zoezi hilo linagusa usalama wa nchi.
“Jambo la msingi
fanyeni kazi kwa ushirikiano na umoja kati ya watendaji wa idara za serikali na
UNHCR, hakuna aliye juu ya mwingine,” alifafanua Marijani.
Alifafanua kuwa, katika
uhuishaji huo zinaweza kutokea changamoto ambapo utatuzi wake unapaswa
kushirikisha viongozi na watendaji wa pande zote.
Afisa Mkuu wa
Uendeshaji, Utawala na Makambi kutoka idara hiyo, Stephen Msangi, alisema wanatarajia
kuhuisha taariza za wakimbizi 231 waliojadiliwa.
Alisema pia kua
wakimbizi 12 ambao wameongezeka hivi karibuni hivyo kufikia idadi ya wakimbizi
243 walioandikishwa ambao taarifa zao zitahakikiwa na kuthibitishwa.
Naye Monday Iddi
ambaye ni Afisa Hifadhi ya Wakimbizi mkoani Kigoma, alisema lengo la uhuishaji huo
ni kufahamu idadi ya wakimbizi waliopo katika mikoa mbalimbali nchini.
“Baada ya uhuishaji,
taarifa zao zitakuwa katika mfumo hivyo watashindwa kujiandikisha zaidi ya mara
moja, uhuishaji huu utahusisha alama za vidole na macho (mboni),” alisema.
Mkimbizi yeyote
ambaye hatajitokeza wakati wa uhuishaji takwimu taarifa zake hazitahuishwa,
usajili wake utasitishwa.
Wakimbizi hao wanatakiwa
kufika na nyaraka za utambulisho zikiwemo barua ya uthibitisho wa mkimbizi,
usajili, kibali cha kuishi nje ya kambi, vyeti vya kuzaliwa.
Nyaraka nyingine ni
vyeti vya ndoa, hati ya kusafiria, vitambulisho vya kazi, shule, chuo na
nyaraka nyingine yoyote inayomtambulisha mkimbizi ambayo inatambulika kisheria.
Shughuli zote
zinazohusiana na uhakiki wa taarifa za mkimbizi na waomba hifadhi zinatolewa
bure ambapo uhuishaji huo hautahusisha wakimbizi wa mwaka 1972.
Wakimbizi hao ni wale wanaotoka makazi ya Ulyankulu,
Katumba, Mishano na waishio vijijini mkoani Kigoma.
No comments:
Post a Comment