WAKATI
Kocha Mwinyi Zahera akihaha kulipwa madai yake ya kuvunjiwa mkataba,
baadhi ya nyota wa kigeni wa Yanga wameripotiwa kuandikia uongozi barua
za kuvunja mikataba yao kwa kile
walichokiita ‘uongozi kutoiheshimu mikataba hiyo’ kwa kutowalipa
mishahara na
stahiki zao nyingine kwa zaidi ya miezi mitatu.
Beki
mahiri wa klabu hiyo, raia wa Ghana, Lamine Moro, alikuwa wa kwanza kabisa
kuripotiwa kuwa amevunja mkataba wake baada ya Yanga kushindwa kumlipa mshahara
wa miezi mitatu.
Hali
hiyo, ilimsukuma Lamine, awasilishe kwa uongozi barua yake ya kuvunja mkataba
wake na Yanga SC, lakini akaenda mbali zaidi kwa kuwasilisha barua hiyo kwa TFF
na kutuma nakala ya barua hiyo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya FIFA.
Baada
ya Lamine kufanya hivyo, kukaibuka wimbi la nyota wa kigeni kadhaa Yanga nao
kufuata nyayo, wengi wakifanya hivyo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa Yanga SC
ilipanga kuwaondoa kundini baadhi ya wachezaji wa nje ambao wameonekana kuwa na
viwango vya wastani ili kupisha wengine.
Imedaiwa
kuwa, Yanga ilipanga ‘kuwachinja’ nyota hao ili kujipa nafasi ya kuongeza
wengine katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo unaotarajia kuanza
Desemba 15, 2019 hadi Januari 15 mwakani, huku ikitegemea nguvu ya tajiri mmoja
ambaye jina lake liko mafichoni.
Kibopa
huyo alikuwa tayari kuwalipa wachezaji hao sehemu ya gharama za kuvunja
mikataba yao kwa maelewano maalum, lakini nyota hao wameshtuka na kuamua
kuchukua hatua, sababu ya kutoaminiwa kwao ikitajwa kuwa ni kutowepo kwa Mwinyi
Zahera aliyewasajili.
Ukiondoa
Lamine Moro, nyota wengine wanaotajwa kuwemo kwenye sakata hili la kutaka
kuondoka kwa kutokuheshimiwa mikataba yao ni pamoja Sadney Urkhob, David
Molinga, Maybin Kalengo, Moustapha Seleman na Issa Bigirimana.
Jitihada
za kuupata uongozi wa Yanga na TFF kuzungumzia sakata hili
hazikuzaa matunda, lakini bado tunaendelea kuwasaka kusikia watasema nini juu
ya mtanziko huo unaokinyemelea kikosi cha Charles Mkwasa.
No comments:
Post a Comment