MFANYABIASHARA
maarufu Marijan Msofe maarufu 'Papaa Msofe' na wenzake wanne
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashitaka matano ikiwemo utakatishaji wa fedha wa zaidi ya Sh.Mil 900.
Si
mara ya kwanza Papaa Msofe kufikishwa mahakamani hapo kwani aliwahi
kukabiliwa na kesi ya Mauaji mwaka 2012 kisha alifunguliwa kesi ya
Kughushi mwaka 2015.
Mbali na Msofe, washitakiwa wengine ni Wakili wa Kujitegeme, Mwesigwa Mhingo,Fadhil Mganga, Wencelaus Mtui na Joseph Haule.
Miongoni
mwa mashitaka yanayowakabili ni Kuratibu Genge la Uhalifu, Utakatishaji
Fedha na Kujipatia Fedha kwa Njia ya udanganyifu.
Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu,
Huruma Shaidi kuwa washtakiwa wametenda makosa yao kwa nyakati tofauti
tofauti.
Katika kosa la kujipatia fedha kwa
njia ya udanganyifu inadaiwa walilitenda kati ya Desemba 2018 na
Septemba 2019, Jiji la Dar es Salaam ambapo wakiwa na nia hiyo
walijipatia Dola za Kimarekani Laki 3 (Sawa na Mil.660) kutoka kwa
Pascal Camille wakidai ni Pesa za kuumuzia madini ya Dhahabu Kilo 200
ambayo wangemsafirishia kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.
Pia
inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya tarehe hizo hizo ambapo
walimlaghai Johnson Mason kwamba watamuuzia Kilo 20 za madini ya
Dhahabu yenye thamani ya Mil.253 kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.
Pia
kosa la utakatishaji fedha inadaiwa walilitenda kati ya Disemba 2018 na
Septemba 2019 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambapo
walijipatia Dola za Kimarekani Laki 3 (Sh.Mil 660) na Dola Laki Moja na
Kumi (Sawa na Sh.Mil 253) ambazo ni zaidi ya Mil.900 huku wakijua fedha
hizo ni zao la udanganyifu.
Washitakiwa hao
hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu kesi hiyo ni ya Uhujumu Uchumi,
hivyo haina dhamana ambapo shauri hilo limehairishwa hadi Desemba 16,
2019.
No comments:
Post a Comment