HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 02, 2019

Papaa Msofe afikishwa mahakamani

Na Janeth Jovin

MFANYABIASHARA maarufu Marijan Msofe maarufu 'Papaa Msofe' na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu  Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwemo utakatishaji wa fedha wa zaidi ya Sh.Mil 900.

Si mara ya kwanza Papaa Msofe kufikishwa mahakamani hapo kwani aliwahi kukabiliwa na kesi ya Mauaji mwaka 2012 kisha alifunguliwa kesi ya Kughushi mwaka 2015.

Mbali na Msofe, washitakiwa wengine ni Wakili wa Kujitegeme, Mwesigwa Mhingo,Fadhil Mganga, Wencelaus Mtui na Joseph Haule.

Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni Kuratibu Genge la Uhalifu, Utakatishaji Fedha na Kujipatia Fedha kwa Njia ya udanganyifu.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa washtakiwa wametenda makosa yao kwa nyakati tofauti tofauti.

Katika kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa walilitenda kati ya Desemba 2018 na Septemba 2019, Jiji la Dar es Salaam ambapo wakiwa na nia hiyo walijipatia Dola za Kimarekani Laki 3 (Sawa na Mil.660) kutoka kwa Pascal Camille wakidai ni Pesa za kuumuzia madini ya Dhahabu Kilo 200 ambayo wangemsafirishia kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.

Pia inadaiwa walitenda kosa hilo kati ya tarehe hizo hizo ambapo walimlaghai Johnson Mason kwamba watamuuzia Kilo 20 za  madini ya Dhahabu yenye thamani ya Mil.253 kwenda Ureno wakati wakijua si kweli.

Pia kosa la utakatishaji fedha inadaiwa walilitenda kati ya Disemba 2018 na Septemba 2019 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambapo walijipatia Dola za Kimarekani Laki 3 (Sh.Mil 660) na Dola Laki Moja na Kumi (Sawa na Sh.Mil 253) ambazo ni zaidi ya Mil.900 huku wakijua fedha hizo ni zao la udanganyifu.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu kesi hiyo ni ya Uhujumu Uchumi, hivyo haina dhamana ambapo shauri hilo limehairishwa hadi Desemba 16, 2019.

No comments:

Post a Comment

Pages