Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza
na wakuu wa vyuo na wakufunzi kutoka Vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi wakati
akihitimisha mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi hao jijini Dar
es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW).
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW).
Na Mwandishi Wetu
Serikali imeanza mpango wa kuwa na vituo vya malezi kwa watoto
nchini nzima ili kuhakikisha wanajamii wanayapa kipaumbele malezi na
makuzi kwa watoto ili kuhakikisha kunakuwa na taifa madhubuti.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema hayo leo
jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Semina ya Mafunzo ya Elimu ya Malezi,
maendeleo na makuzi kwa wakufunzi kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Dkt.
Jingu amesema kuwa vituo hivyo vitaratibiwa na Serikali ila
vitaendeshwa na kusimamiwa na wananchi katika maeneo yao na mpaka sasa
kuna zaidi ya vituo 1500 nchi nzima na vingine vinaendelea kuanzishwa.
Ameongeza kuwa malezi ni msingi mkubwa katika kuhakikisha
tunapata kizazi chenye maadili, uwajibikaji na uzalendo katika kizazi
itakayosaidia kujenga taifa bora.
"Mafunzo haya ni muhimu na mmeamua suala sahihi, watoto
wanahitaji malezi ya karibu na sio malezi tu bali wapate malezi sahihi"
alisema Dkt. Jingu
Dkt. Jingu pia amewataka washiriki wanatumia stadi hiyo
kuisaidia jamii na nchi kuweza kuwa na muelekeo mzuri kwa kuwa na vijana
wazalendo wawajibikaji kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi kutoka Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde amesema kuwa Wizara ya Elimu
itahakikisha inashirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha Elimu ya
Malezi, maendeleo na makuzi kwa watoto inatekelezwa.
Ameongeza kuwa Wizara ya Elimu imehakikisha kila Chuo cha
Maendeleo ya wananchi kinakuwa na kituo cha kulea watoto ili kuhakikisha
inawasaidia watoto.
Naye Mwakilishi wa washiriki ambaye ni Mkuu wa Chuo cha
Maendeleo ya Jamii Mbinga Bw. Lotty Mwang'onda amesema kuwa mafunzo
waliyoyapata yatawasaidia kuleta mabadiliko hasa katika jamii inayowazunguka
katika vyuo vyao ili kuhakikisha malezi, maendeleo na makuzi yanazingatiwa
katika ukuaji wa mtoto.
Ameongeza kuwa wao kama washiriki wameshukuru kwa uzoefu na kama
wataalam wa wanaofanya kazi na jamii watashirikiana na jamii kuhakikisha elimu
walioyoipata inawafikia jamii inayowazunguka.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Karibu Tanzania KTO Bw. Aidan
Mchawa ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa ushirikiano wao na asasi za
kiraia katika kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi na kuhakikisha program ya
Malezi, maendeleo na makuzi ya awali ya mtoto inarudisha
misingi ya malezi ya mtoto hasa wa kitanzania.
Naye mshiriki Bi. Felister Nanguka ameishukuru Serikali kwa kuwezesha
upatikanaji wa elimu ya mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi katika jamii
hasa vijijini na kuahidi kufanya kazi hiyo kwa nguvu zao kwa kukaza msuli ili
kuhakikisha watoto wanapata malezi stahili.
Shirika la Karibu Tanzania KOT limeandaa mafunzo kwa wakufunzi
kutoka vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo
kuhusu malezi, maendeleo na makuzi ya awali ili wakaitoe elimu hiyo kwa jamii
inayowazunguka.
No comments:
Post a Comment