Na Tiganya Vincent
MKUU wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri amepiga marufuku watu wazima na vijana kucheza michezo mbalimbali
ikiwemo ‘pool’, bao na karata nyakati za asubuhi ili waweze kutumia muda huo kwenye shughuli za kilimo na
uzalishaji mali.
Hatua hiyo itasaidia
kukabiliana na uzururaji na uzembe unaofanywa na baadhi ya vijana nyakati
ambazo wanatakiwa kuwa shambani kulima mazao mbalimbali kwa ajili ya maendeleo
yao.
Mwanri alitoa kauli hiyo hivi
karibuni Wilayani Kaliua wakati wa ziara yake ya kuhamasisha kilimo bora na
ufanyaji wa kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Alisema watu wanaoshinda
wakicheza michezo mbalimbali wakati wenzao wako mashambani wakilima ndio
wanakuwa wa kwanza kudai chakula cha msaada pindi wanapokabiliwa na njaa.
Mwanri aliwataka viongozi
kuanzia ngazi ya Wilaya hadi vitongoji kuhakikisha hakuna vijana ambao watakuwa
mitaani wakicheza michezo mbalimbali wakati wanapaswa kuwa shambani.
Aliongeza kuwa watu wa aina hiyo ndio wanasababisha
ucheleweshaji wa maendeleo na wakati mwingine wanakuwa wa kwanza kuomba chakula
cha msaada pindi wanapokuwa hawana chakula.
“Ni marufuku kucheza
pool, karata na bao wakati huu…ni lazima watu wote wenye uwezo wa kufanyakazi
wawe mashambani…michezo hiyo ianze nyakazi za jioni…tukiendekeza michezo hiyo
nyakati za kilimo Tabora tutabaki watazamaji wa maendeleo wakati mingine
inapiga hatua sisi tutabaki kulalamika kwa sababu ya kuendekeza michezo nyakati
za kilimo” alisema.
Mkuu wa Mkoa huyo
aliongeza kuwa baadhi ya watu wa aina hiyo wakati mwingine ndio wanahisiwa
kujihusisha na vitendo vya uharifu ikiwemo wizi na ukabaji kwa kuwa hawana
shughuli ya kupatia kipato halali.
“Hivi kijana ambaye kila
siku yuko kwenye bao, karata anapata wapi pesa za kujikimu yeye na familia yake
ni lazima tujiulize…vijana ndio wazazi wa sasa wanajibika kubeba majukumu
ikiwemo kufanyakazi kwa bidii kwa ajili ya ustawi wao na watoto wao”alisisitiza.
Alisema ni lazima kila
mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi kuhakikisha kuwa anafanyakazi halali na kuwa na
uhakika wa chakula cha kutosha na kuwa na ziada itakayomsaidia katika shughuli
za maendeleo yake.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akionyesha mfano kwa vitendo kwa
Wanakijiji wa Ibambo wilayani Kaliua juu ya palizi bora ya mimea wakati
wa ziara yake ya siku nne ya kuhamasisha kilimo bora ikiwemo cha pamba
hivi karibuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Dkt. John Pima akitoa ufafanuzi kabla ya ya kumkaribisha Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ili atoea elimu kwa Wanakijiji wa
Ibambo wilayani Kaliua juu ya palizi bora ya mimea wakati wa ziara yake
ya siku nne ya kuhamasisha kilimo bora ikiwemo cha pamba hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment