December 12, 2019

TAKUKURU YAMSHIKILIA KATIBU WA CCK

Na Tatu Mohamed

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Ilala inamshikilia Katibu Mkuu Wa Chama cha Siasa cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi kwa kosa kujifanya mtumishi wa Taasisi hiyo na kuomba rushwa ya Sh. Milioni 50.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Christopher Myava alisema Muabhi alijifanya taasisi hiyo na kuomba rushwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Bharya Engeneering & Contracting Company Limited (BECCO) iliyopo Vingunguti, jijini Dar es Salaam, Manraj Bharya. 

Myava alisema uchunguzi wa Takukuru umebaini kwamba Muabhi dhumuni lake lilikuwa kuomba rushwa hiyo ili amsaidie Bharya katika tuhuma zake zilizokuwa zinamkabili Independent Power Tanzania Limited. 

"Mtuhumiwa alikamatwa Disemba 10 majira ya jioni katika ofisi za kampuni ya BECCO akiwa amepokea fedha za mtego wa rushwa kiasi cha Sh. 100,000," alisema. 

Aliongeza kuwa uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili sheria ichukie mkondo wake. 

"Natoa rai kwa wananchi kujihadhari na matapeli wa aina hii na kujiepusha nao, na endapo wakibaini wahalifu wowote wa namna hii watoe taarifa Takukuru ili uchunguzi ufanyike na watuhumiwa waweze kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages