HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 17, 2019

THE DESK & CHAIR FOUNDATION YASAIDIA JAMII VISIMA VYA MAJI 436

Picha ya Maktaba
KATIKA kukabiliana na tatizo la maji, Taasisi ya Desk & Chair Foundation nchini, imechimba na kukabidhi kwa wananchi visima 436, ili kuwaondolea changamoto hiyo.

Imeelezwa visima hivyo vimesaidia wanawake wengi na wasichana, kutokutembea umbali mrefu kufuata maji, pamoja na kuiepusha jamii kunywa maji yasiyokuwa safi na salama.


Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Alhaj Sibtain Meghji, wakati akikabidhi kisima cha maji safi kwa wana Kijiji wa Karumo, Wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza.


Kisima hicho kilichangiwa na vijana wa Hussein Inspires Group of Muslim, Jumuiya ya KSI (Mwanza) Jamaat na baadhi ya washiriki wa kikundi hicho.


Meghji alisema wananchi wa Kijiji hicho cha Karumo kabla ya mradi huo, walikuwa wakitembea umbali wa kilometa 20 kufuata maji, hali iliyokuwa na athari kwao.


"Maji ni uhai. Ndiyo leo hii uongozi wa Desk & Chair Foundation unawakabidhi mradi huu wa maji. Kutembea umbali mrefu kufuata maji inaathiri pia shughuli nyingine za uzalishaji mali.


"Wanafunzi 1,000 wa shule za msingi, wanafunzi wa mafunzo ya ufundi stadi na familia 50 za karibu, watanufaika kutoka kisima hiki kila siku," Alhaj Meghji alisema na kuhimiza kutunzwa kwa kisima hicho.


Kulingana na kiongozi huyo wa Taasisi ya Desk & Chair Foundation Tanzania, mradi huo wa maji utasaidia kupunguza adha na magonjwa yanayosababishwa na unywaji maji machafu.


Alisema kuingia ndani ya Ziwa Victoria kuchota maji ya kunywa majumbani, husababisha baadhi yao kushambuliwa na viboko, magonjwa ya kichocho na homa ya matumbo.


Alisema kisima hicho kitasaidia mazingira salama zaidi kwa vijana wa kike, ambao awali walikuwa wakishambuliwa na watu wasiojulikana wakilazimishwa kutoa heshima zao.


Meghji aliwashukuru wahisani wa Taasisi ya Desk & Chair Foundation kwa misaada yao, wanayoitoa kusaidia kutatua kero zinazoiegemea jamii yenye mahitaji muhimu nchini.

"Wamekuwa msaada mkubwa sana kusaidia jamii. 


Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awalipe mema wahisani wetu na Watanzania wote," alisema kiongozi
huyo.


Katika makabidhiano hayo ya kisima cha maji, wakazi wa Kijiji cha Karumo waliupongeza uongozi wa Desk & Chair Foundation kwa msaada huo wa mradi.


Walisema kabla ya kisima hicho walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata maji, jambo lililokuwa likiharibu shughuli nyingine za kiuchumi.


"Tumefurahi mno. Mungu awabariki," alisikika mwana mama Janeth Kasungwa, huku akihimiza wenzake kutunza kisima hicho ili kidumu na kiwasaidie zaidi.


Mbali na uchimbaji visima vya maji maeneo mengi nchini, Taasisi hiyo ya Desk & Chair Foundation, imekuwa ikishiriki pia kusaidia vituo vya afya, jamii yenye matatizo.


Changamoto nyingine inazokabiliana nazo ni vyoo shuleni, hospitalini usaidizi wa matibabu kwa watoto wanaosumbuliwa na magonjwa bila wazazi wao kuwa na uwezo, pamoja na watu wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment

Pages