December 20, 2019

TUZO ZA MUZIKI WA DANSI KUTOLEWA KESHO, NANI KUIBUKA KIDEDEA?

Na Sitta Tumma, Mwanza

WANAMUZIKI wa dansi nchini, wameshauriwa kuboresha kazi zao, ili kukubalika zaidi kwenye soko ulimwenguni kote.
Aidha, wametakiwa kutumia fursa wanazopata katika fani hiyo, zikiwamo tuzo ili katika kuutangaza muziki wa dansi kwa manufaa yao.

Mwandaaji wa tuzo za muziki wa dansi Tanzania, dhidi ya wanamuziki waliofanya vizuri mwaka 2019, Bernard James, amesema hayo jijini Mwanza, muda mfupi uliopita.

Tuzo hizo za muziki wa dansi ambazo ndiyo mara ya kwanza kutolewa nchini, zimeandaliwa na Kampuni ya Cheza Kidansi Entertainment ya jijini Mwanza.

Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi , juu ya tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa saa 2:00 usiku kesho, Bundesiliga Hotel, alisema tuzo hizo ni muhimu.

"Wanamuziki wanatakiwa kufahamu kuwa kupitia tuzo hizo, wao na muziki huo wanapata kufahamika zaidi.

"Hii inaasisi maboresho zaidi ya mziki wa dansi ambao pia ni ajira kwa wasanii wake," alisema James.

"Hivyo, yawapasa kufanya uwekezaji kupitia matamasha, vyombo vya habari na mialiko mbalimbali, ili kuwaongezea kipato," alisisitiza.

James aliwakaribisha wakazi wote wa Mwanza na Kanda ya Ziwa, kufika Bundasliga kujionea burudani itakayooneshwa na bendi mbalimbali.

Shughuli ya utoaji wa tuzo hizo za muziki wa dansi, utahudhuriwa na wasanii mbalimbali, wakiwamo wakongwe na bendi tofauti zitatumbuiza.

Kwa mujibu wa James, tuzo 13 zitatolewa kwa wasanii mbalimbali, zikiwamo bendi na watunzi bora wa muziki huo unaopendwa na watu wa rika lote.

"Tuzo hizi zinaongeza ushindani na kusababisha ubunifu kuwa mkubwa. Ukiwapo fanisi utaongeza bidii na kipato," alisema.

Alisema bendi zitaonesha ufundi jukwaani zikiongozwa na Bogoss Musica, inayomilikiwa na Nyoshi El Saadat.
Alisema tuzo za waandishi wa habari na watangazaji wa muziki wa dansi, zitaasisiwa ili kukuza muziki huo.

James anayehusika na uandaaji wa tuzo hizo za dansi, aliwaomba waandishi wa habari jijini Mwanza kufika kwa wingi katika hafla hiyo, ili kuuhabarisha umma yatakayojiri.

No comments:

Post a Comment

Pages