December 09, 2019

Waandishi wa habari wanawake watakiwa kuacha uoga

Na Mwandishi Wetu
 
WAANDISHI wanawake nchini wametakiwa kuacha uoga na kusimamia haki zao wanapokua katika sehemu zao za kazi ili Kuondokana na changamoto zinazowakabili ikiwamo vitendo vya kikatili ndani ya vyumba vya habari.

Hayo yamebainishwa  jijini  Dar es Salaam jana na Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia, Simbalache Msasanuru
wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari juu ya masuala ya Usawa wa kijinsia na Usalama  sehemu za Kazi iliyoandaliwa na Chama cha wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini (JOWUTA).

Msasanuri anasema ili kuondokana na matatizo yanayowakumba waandishi was habari kwenye vyumba vya habari ni kuacha uoga kwa kuvunja ukimya pindi wanalofanyiwa vitendo visivyo faa ikiwemo kuombwa rushwa  ya Ngono.

Anasema mara nyingi watu wanaowaomba waandishi hao rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari hawahusiki katika nafasi za maamuzi za kutoa ajira aukumfukuzisha kazi.

"Waandishi wamekua mstari wa mbele kuandika habari namna ya watu wanavyonyanyaswa au kunyimwa mishahara na kushindwa kujisemea wenyewe wanavyokumbana na changamoto mbalimbali sehemu zao za kazi,"anasema

Msasanuru anasema ni vema waandishi wa kada hiyo wakapunguza Kuchekana na kuoneana wivu badala yake waungane na kuwa kitu kimoja Katika kutetea masilahi yao.

"Hakikisheni mnakuwa sio miongoni mwa watu wa kushawishi vitendo vya kikatili kufanyiwa hivyo mnatakiwa kuvaa vizuri sehemu zenu za kazi na kuhakikisha mnajituma bila kuchoka hii itakuwa njia ya kuondoa rushwa ya ngono katika vyumba vingi vya habari,"anasema

Kwa Upande wake Katibu wa JOWUTA, Suleiman Msuya anasema waandishi wa habari wamekuwa wakiandika matatizo yanayowakabili watu wengine na kujisahau wao wenyewe.

Anasema Chama hicho kipo nchi nzima na kusaidia waandishi katika sehemu zao za kazi na kuhakikisha kinakuwa na uwiano mmoja katika kazi Kati ya mwandishi wa kiume na wakike.

"Hadi sasa tunawanachama takribani 130 nchi nzima wote wakiwa waandishi na kinalenga kusimamia maslahi ya waandishi katika sehemu zao za kadi,"anasema Msuya.

No comments:

Post a Comment

Pages