December 09, 2019

WANAHARAKATI WATAKA MADAWATI YA KIJINSIA NGAZI YA MITAA

Na Tatu Mohamed
WANAHARAKATI mbalimbali wameomba elimu kuhusu masuala ya ukatili wa jinsia iendelee kutolewa kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu, ili kuweza kuvitokomeza vitendo hivyo.
Pia wanaharakati hao wameomba kuanzishwa kwa madawati ya kijinsia kuanzia katika serikali za mitaa.
Hayo waliyabainisha mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika muendelezo wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambazo huratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) na hufanyika kila Jumatano.
Mwanaharakati Anna Kikwa akizungumza kwenye semina hiyo iliyobeba ujumbe ‘Nafasi ya jamii katika vita ya kutokomeza ukatili wa kijinsia’, alisema elimu inahitajika kwa kushirikana na wadau wengine ili kuleta nguvu ya pamoja.
“Ili tufanikiwe katika kupinga ukatili wa kijinsia tunapaswa kufanya kwa pamoja, jamii, wadau ili kutokomeza matukio ya ukatili,” alisema Kikwa.
Naye Mwanaharakati Janeth Mawinza alisema kuanzishwa kwa madawati ya kijinsia kuanzia ngazi ya mitaa itasaidia taarifa kutolewa bila vikwazo.
Alisema baadhi ya wanakumbwa na ukatili huo wanapatwa na woga wa kufika polisi na kwamba unazishwaji wa madawti mtaani kutaongeza takwimu za taarifa zinazotokea kwenye jamii.
“Kuwepo na motisha wa wanaharakati ambao wamekuwa wakipambana na hata kuhatarisha maisha yao, binafsi nilifikia kuhatarisha maisha wakati nikifuatilia kesi fulani kuhusu ukatili wa kijinsia,“ alisema Mawinza.

No comments:

Post a Comment

Pages