HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 12, 2020

UBA yazindua akaunti mpya nne

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza katika uzinduzi wa huduma nne za Benki y UBA jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Benki ya UBA Usman Isiaka.


Na Irene Mark

 BENKI ya UBA imezindua huduma nne mpya za akaunti maalum kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya kibenki ya wateja wake kulingana na umri na vipato vyao. 
Huduma hizo za akaunti pia zinalenga kurahisisha mahitaji ya wateja wa benki hiyo ya kifedha ya sasa na baadae.
Akaunti hizo ni UBA Malaika, UBA Janja, UBA Kizazi Kipya na UBA Hazina.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Rejareja Benki ya UBA, Geofrey Mtawa alisema akaunti ya UBA Malaika inawalenga wazazi wanaotaka kuwawekea pesa watoto wao kabla hajazaliwa hadi miaka 12.
Kuhusu UBA Janja alisema ni maalumu kwa vijana wanaoanzia miaka 13 hadi 17 wakati UBA Kizazi Kipya ni kwa vijana walioanza kujiwekea akiba wakiwa na miaka 18 hadi 25. 
Kwa mujibu wa Mtawa, UBA Hazina inawalenga vijana wa miaka 25 na kuendelea kwa kuwa ni maalaum kwa ajili ya watu kwenye rika la kutaka kutimiza ndoto zao, wanaojiwekea akiba  ili kukidhi mahitaji yao ya shule, ujenzi au biashara.
“Huduma hizi ni utekelezaji wa malengo yetu ya kuwa benki kinara kwa kutoa huduma bora za kibenki kwenye soko kwa kuzingatia maombi na mahitaji ya wateja wetu, UBA tumeendelea kuvumbua huduma zinazorahisisha upatikanaji wa fedha,” alisema Mtawa.
Hii sio mara ya kwanza UBA ikiongoza kwenye kuanzisha huduma bora za kibenki zenye kuleta mapinduzi yenye tija sokoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya UBA Tanzania, Usman Isiaka alisema benki yake inalenga kurahisisha maisha ya kibenki na kuwapa wateja huduma bora zenye ushindani mkubwa kwenye soko.
“Uanzishaji wa huduma hizi unaendana na falsafa yetu ya UBA ya kumuweka mteja mbele, ambapo benki inafanya vitu sio kwa jinsi inavyotaka bali kwa jinsi wateja wetu wanavyotaka, muda wanaotaka na kwa njia wanayotaka ziwe, ndio maana tukaangalia rika zote na kuhakikisha hatujamucha mtu yeyote kuanzia mtoto akiwa tumboni, mwanafunzi wa shule, chuo, wafanyakazi, wafanyibiashara na hata kizazi cha kuanzia miaka 25 na kuendelea," alisisitiza Isiaka.

No comments:

Post a Comment

Pages