Waziri wa Kilimo Japhet
Hasunga akizungumza na Vijana Zaidi ya 700 waliohudhuria uzinduzi wa Kitaifa wa
Kongamano la Vijana katika Kilimo lililofanyika Mkoani Songwe ambapo amewataka
Vijana kujikita katika Kilimo kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Kilimo
imeanzisha Mpango wa kutumia Vijana katika kuendeleza sekta ya Kilimo Nchini
kwakuwa wao ni nguvu kazi ambayo inaweza kuleta mabadiliko ya haraka.
Waziri wa Kilimo Japhet
Hasunga ameyasema hayo mapema leo wakati akizindua Kongamano la Vijana katika
Kilimo lililozinduliwa kitaifa Mkoani Songwe na kushirikisha Vijana kutoka
Mikoa ya Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi.
“Wizara ilifanya tathmini
na kuona kuwa licha ya mambo mazuri tunayofanya, inabidi katika mikakati yetu
tuwe na Mkakati wa Kuwatumia Vijana ili waingie katika Kilimo.”, amesema Waziri
Hasunga.
Ameongeza kuwa ili
kufanikisha Mpango huo Wizara ya Kilimo itahakikisha ardhi inayofaa kwa Kilimo
inapatikana na Kutengwa kwa kuwa na sheria ya kutenga ardhi ya Kilimo, pia
Mikoa inapaswa kutenga maeneo yanayo faa kwa ajili ya Kilimo.
Waziri Hasunga amesema
Wizara pia itahakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha, pembejeo na zana za
Kilimo, Miundombinu ya Umwagiliaji inawekwa kwakuwa Mvua ikizidi au kupungua ni
hasara kwa Mkulima pamoja na kufundisha mbinu na ujuzi wa ujasiriamali katika
kilimo kupitia Makongamano.
Amesema Wizara inatambua
kuwa Vijana ndio nguvu kazi huku takwimu zikionyesha kuwa asilimia 96 ya
watanzania hawaja ajira hivyo, hiyo ni nguvu kazi ambayo inatakiwa ielekezwe
katika Kilimo.
Waziri Hasunga ameongeza
kuwa Wizara ina tambua changamoto zilizopo katika sekta ya Kilimo na tayari
imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kusajili
wakulima ili watambulike kwa urahisi, kusajili waadau wa Kilimo na Kuanzisha
Bima ya Mazao.
Aidha amewataka vijana
wote kubadili mtazamo kuwa kilimo ni kushika jembe la Mkono kwakuwa Kilimo ni
sekta pana inayojumuisha kulima, kusindika na kuongeza thamani ya mazao,
masoko, uhifadhi na pembejeo hivyo wasiache kujikita hata katika moja ya fursa
hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amesema Mkoa wa Songwe ni moja kati ya wazalishaji wakubwa wa Chakula
Nchini ambapo uzalishaji unafanyika ajili ya Chakula na Kuuza ndani na nje ya
nchi pia uhakika wa kuvuna kwa wingi chakula mwaka huu ni mkubwa.
Brig. Jen. Mwangela
amesema Mkoa una Hekta Milioni mbili ambapo zinazotumika katika Kilimo ni
asilimia 30 tu huku eneo lingine likitumika katika makazi na Misitu lakini eneo
kubwa linalobaki halijatumika bado.
Ameongeza kuwa Mkoa una
eneo la hekta elfu 18 linalofaa kwa ajli ya kilimo cha Umwagiliaji na pia
amewahakikishia vijana kuwa ardhi kwa ajili ya Kilimo Mkoa wa Songwe sio tatizo.
Brig. Jen. Mwangela amesema
vijana wabadilike kifikra na kuanza kuthamini kilimo kwakuwa ili kupambana na
umasikini vitendo vinahitajika Zaidi kuliko maneno tu ya kulalamika.
Naye Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Songwe Eliniko Mkola amesema vijana wa Kitanzania waliopata mafunzo ya
Kilimo Nchini Israel wasikae na elimu hiyo bali wawaelimishe vijana wenzao na
mashamba yao yatumike kama madarasa ya kujifunzia Kilimo.
Mkurugenzi wa SUGEC
Revocatus Kimario amesema taasisi yake inajihusisha na kuwasaidia vijana katika
Sekta ya Kilimo na moja ya changamoto ni mtamzamo wa vijana juu ya kilimo.
Kimario amesema walimu pia
wamechangia kutengeneza mtazamo hasi juu ya kilimo kwa kuwa wamekuwa wakitoa
adhabu zinazohusiana na Kilimo pale ambapo mwanafunzi anafanya makossa.
“Vijana hawapendi kilimo
kwakuwa wamezoe kulima kama adhabu wanapokuwa shuleni, unataka akimaliza masomo
akafanye kitu ambacho amekijenga kuwa ni adhabu?, Kilimo ni ajira hivyo waalimu
wanapaswa kuacha kukitumia kama adhabu kwa wanafunzi.”, amesema Kimario.
Katibu wa Umoja wa Vijana
wa CCM Mkoa wa Songwe Hassan Lyamba ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa
Kongamano hilo kwakuwa litawafungua akili vijana juu ya fursa mbalimbali
zinazopatikana katika sekta ya Kilimo.
Lyamba ameongeza kwa
kuwataka vijana kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo yale yote waliyo jifunza
katika kongamano hilo ili wawe sehemu ya mabadiliko katika sekta ya Kilimo
nchini.
Kauli Mbiu ya Kongamano la
Vijana ambalo linatarajiwa kufanyika nchini Kote katika Kanda Saba ni; “Vijana,
Kilimo ni Ajira”.
No comments:
Post a Comment