*Asema wenye maambukizi wamefikia 480 ikiwa ni
ongezeko la wagonjwa 196
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wagonjwa
167 wamepona ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa virusi vya corona
(COVID-19) na ameendelea kuwasisitiza Watanzania wachukue tahadhari ya kutosha
na wafuate ushauri wa Wataalamu wa Afya na maelekezo ya Serikali.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuanzia
tarehe 23 hadi 28 Aprili, 2020 wamepatikana watu wengine wapya wenye maambukizi
ya Corona 196 (Bara 174 na Zanzibar 22 ambao walitangazwa na Waziri wa Afya wa
SMZ) na kufanya jumla ya wenye maambukizi nchini kuwa 480.
Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo ya mwenendo
wa ugonjwa wa COVID-19 nchini leo (Jumatano, Aprili 29, 2020) kwenye viwanya
vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma wakati akikabidhi magari ya
kubebea wagonjwa kwa wabunge. Pia amesema mbali na magari hayo kutolewa kwa
ajili ya kuboresha huduma za mama na mtoto yatatumika kuwahudumia wagonjwa wa COVID-19.
“Tarehe 24 Aprili Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto aliwatangaza jumla ya waliopona kuwa ni 37 na
hivyo kufanya jumla ya waliopona kuwa 48. Leo tunafurahi kusema kuwa idadi ya
waliopona imeongezeka kutoka 48 na kufikia 167 (Zanzibar 36 waliotanganzwa jana
na Waziri wa Afya - SMZ na Bara 83).”
“Tunasikitika kueleza kuwa tuna ongezeko la
vifo sita na kufanya jumla ya vifo sasa kuwa 16. Hata hivyo kati ya wenye
maambukizi 297 waliobaki, watu 283 wanaendelea vizuri sana na watu 14 wako
chini ya uangalizi maalum na tunaendelea kuwaondoa walio karibu na wagonjwa
(contacts) walio karantini baada ya kumaliza siku 14.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa hadi tarehe 28
Aprili, 2020 watu 644 wameruhusiwa, ambao wanatoka katika mikoa ya Zanzibar,
Dar-es-Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Kagera, Dodoma, Kigoma na
Songwe.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi wachukue
tahadhari kuhusu taarifa za upotoshaji kwani kwa sasa kumeibuka tabia ya watu
kutoa takwimu zisizo sahihi kuhusu vifo vitokanavyo na ugonjwa wa COVID-19 ambazo
zinasababisha mtafaruku usio wa lazima katika jamii.
“…Sio kila kifo ni cha
Corona, tunasahau kuwa magonjwa mengine yanaua pia sio kila anayeugua na
anayekufa ni corona tuna malaria, BP, kisukari, ukimwi ni magonjwa yanayoua. Tuache
tabia ya kupotosha umma. Tuwaache wataalam wetu wafanye kazi zao.”
“Kwa wale ambao
hawana maambukizi waendelee kufanya kazi zao, mkulima aende akalime tupate
chakula cha kutosha, waliko maofini wawajibike kufanya kazi, waliopo viwandani
wafanye kazi na kila mmoja na sekta yake kama unafanyabiashara sokoni toa
huduma ili wananchi wasikose kupata huduma wanazozihitaji.”
Hata hivyo, Waziri
Mkuu ameendelea kuwasisiza Watanzania wazingatie maelekezo yanayotolewa na
Serikali katika kujikinga na COVID-19 ikiwa ni pamoja na kujiepusha na
misongamano. “Tukizingatia makatazo na maeneo yenye tahadhari tutaishinda vita
hii dhidi ya ugonjwa huu.”
No comments:
Post a Comment