*AKABIDHI MAGARI 10 YA KUBEBEA WAGONJWA KWA WABUNGE
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi magari
10 ya kubebea wagonjwa kwa wabunge ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za dhati za
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha
Watanzania wanapata huduma bora za afya karibu na makazi yao.
Magari hayo 10 ni kati ya magari 50 ya kubebea
wagonjwa yenye thamani ya sh. bilioni sita yaliyonunuliwa na Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Global Fund. Kati ya magari
hayo, 18 yatapelekwa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa na 32 ni kwa ajili ya
hospitali za Halmashauri pamoja na vituo vya afya.
Waziri Mkuu amekabidhi magari hayo leo
(Jumatano, Aprili 29, 2020) kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa
jijini Dodoma. Ambapo amesema mbali na magari hayo kutolewa kwa ajili ya kuboresha
huduma za mama na mtoto pia yatatumika kuwahudumia wagonjwa wa corona ili
kuokoa maisha ya wananchi.
“Eneo hili tumeliwekea nguvu za kutosha na
Watanzania wote ni mashahidi kwa namna ambavyo Serikali imejitahidi sana katika
kupunguza vifo vya mama na mtoto kwenye jamii zetu. Magari haya yatakwenda
kutumika kwa ajili ya mama na mtoto lakini kwa kuwa gari litakuwepo kituoni
litawahudumia na wagonjwa wengine.”
Waziri Mkuu amewashukuru wabunge wote kwa
namna wanavyoishauri Serikali katika kufanya maboresho ya sekta mbalimbali za
maendeleo ikiwa ni pamoja na sekta ya afya ambapo leo wameshuhudia matunda ya
ushauri wanaoutoa.
“Magari haya yatakwenda kufanya kazi ya
kuokoa maisha ya Watanzania wengi kwa kuwasafirisha wagonjwa wa rufaa kutoka
kituo cha afya kwenda hospitali ya wilaya na hospitali ya wilaya kwenda
hospitali ya rufaa.”
Kwa
upande wake,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema
ununuzi wa magari hayo ni utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli
za kuboresha zaidi huduma afya kwa wananchi.
Waziri Ummy amesema Wizara imenunua magari
hayo ili kuimarisha huduma za rufaa kwa wagonjwa hususani kwa akina mama
wajawazito hata hivyo kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona pia magari
hayo yatatumika kwa ajili ya kubebea wagonjwa wa corona.
“Watanzania wameshuhuduia kazi kubwa na nzuri
inayofanywa na Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, wameshuhudia
upatikanaji wa dawa, wameshuhudia maboresho makubwa katika upatikanaji wa vifaa
tiba, ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa hosptali za halmashauri pamoja na
hospitali za rufaa za mikoa na uboreshwaji wa miundombinu ya kutolea huduma za
afya.”
Akizungumza kwa niaba ya wabunge waliopokea
magari hayo, Mbunge wa Ileje, Janneth Mbenne amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa
kitendo hicho cha kihistoria. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa mawazo na maono
makubwa ya maendeleo ya Taifa. Magari haya yatakwenda kuboresha huduma za afya
katika majimbo yetu.”
Naye Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto ameishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015-2020 kwa
vitendo. “…moyo usio na shukurani hukausha mema yote na heri wale wanaowajali
wagonjwa kwa maana ufalme wa Mungu ni wao.”
Pia, Mbunge wa Nyasa na Naibu Waziri wa
Wizara ya Viwanda na Biashara, Stella Manyanya amesema kwa niaba ya wananchi wa
wilaya ya Nyasa wanamshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa msaada huo kwani walikuwa
na changamoto kubwa na gari la kubebea wagonjwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum,
Amina Makilagi wakati alipokabidhi magari 50 ya kubebea wagonjwa kwa
wabunge yenye thamani ya shilingi bilioni 6, Aprili 29, 2020.
Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu,
Mlimwa jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) wakifurahia
wakati Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta (kulia) alikionyesha ufunguo wa
gari la kubebea wagonjwa baada ya kukabidhiwa wakati Waziri Mkuu
alipokabidhi magari 50 ya kubebea wagonjwa kwa wabunge yenye thamani
ya shilingi bilioni 6, Aprili 29, 2020. Makabidhiano hayo yalifanyika
kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment