May 03, 2020

Baraza la madiwani Kalambo laazimia kuwafukuza kazi watendaji wezi

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichon
 Baadhi ya Madiwani waliohudhuria Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo.
 
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Daudi Sichone ametangaza kuwafukuza kazi pamoja na kuwapeleka mahakamani watendaji wa vijiji wanaokusanya mapato na kutowasilisha mapato hayo benki kwaajili ya utekelezaji wa matumizi mbalimbali ya halmashauri hiyo.
 
Amesema kuwa tabia hiyo ilianza kwa watendaji wachache kutumia fedha wanazokusanya hali iliyopelekea na watendaji wengine kuiga tabia hiyo na matokeo yake kuwa desturi kwa watendaji hao kutumia fedha za makusanyo huku ikisomeka kuwa ni wadaiwa (defaulters) jambo ambalo Mwenyekiti huyo analipinga na kusema watendaji hao sio wadaiwa bali ni wezi wa fedha za halmashauri na hivyo wachukuliwe hatua kama wezi. 

“Imekuwa Shida, kuna watendaji ambao sasa hivi wanaona kuwa TAKUKURU nako ni kama nyumbani, na sisi njia nyingine ambayo tunayo, nguvu yetu tuliyonayo ni ya kuwafukuza tu na kuwapeleka mahakamani, kwasababu hatuna namna, tumewapeleka kwenye vyombo ambavyo ndio tunavitegemea, zimefanya kazi yake kwa nguvu zote, tumekwenda hivyo lakini…” Alisema. 

Aliongeza kuwa kuna baadhi ya watendaji wadaiwa ambao wameshajiandikisha ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kalambo ili ifikapo tarehe 30.05.2020 wawe wamemaliza kulipa fedha hizo na kushauri kuwa watendaji hao wasisubiriwe hadi ifike tarehe hiyo, kwani kuna watendaji ambao madeni yao ni makubwa na hivyo hawataweza kulipa fedha hizo kwa pamoja na kuitaka ofisi hiyo kuweka utaratibu wa watendaji hao kulipa kidogokigdogo. 

Maamuzi hayo yalifikiwa na Mwenyekiti huyo baada ya kukubaliana katika vikao vya kamati ya fedha, Uongozi na Mipango jambo ambalo liliungwa mkono na waheshimiwa madiwani wote waliohudhuria katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo tarehe 2.5.2020 kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini. 

Awali akichangia hoja ya kuchukuliwa hatua za kufukuzwa watendaji hao, Diwani wa kata ya Mambwenkoswe, Edwin Msipi alisema kuwa halmashauri hivi sasa inasota kutokana na fedha nyingi kuwemo katika mifuko ya watendaji na hivyo kupelekea miradi mingi ya halmashauri kushindwa kutekelezeka na hivyo kulitaka baraza hilo kuwa na mkakati wa kuwashughulikia watendaji hao.

“Kwakweli tuna-suffer kwenye halmashauri hii, kama halmashauri zote za Tanzania ziko hivi sijui, ila tunasota na pesa zipo kwa watu ambao walipoanza kuiba kidogo kidogo ikawa ni fundisho hata kwa wengine sasa, kwamba aah, sisi kule si tunadaiwa tu, tutapeleka nusu nusu, mkakati haujafanyika isipokuwa tukizungumza kwenye chemba kama hivi, tunazungumza lakini yataishia hapa hapa,” Alisisitiza. 

Katika maelezo yake Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ambaye ni mwalikwa wa kikao hicho alisema kuwa jukumu la kwanza la madiwani ni kusimamia ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na kuongeza kuwa hao wadaiwa (defaulters) ni wa kwao na wapo ndani ya uwezo wao na kuwathibitishia kuwa endapo watahitaji msaada wa serikali, ofisi yake na ofisi ya mkuu wa Wilaya zipo tayari kutoa msaada huo. 

“Kwahiyo tunataka kwa mkoa mzima milioni 450 ziwe zimeshakusanywa na kulipwa waheshimiwa madiwani, kufikia mwisho wa mwezi huu, kwahiyo ni lazima tupambane kufa na kupona na hawa ‘defaulters’, sio tu kuwafunga lakini kwanza wairudishe hiyo hela ili tupate hela ya kuwalipa madiwani, halafu hatua nyingine itafuata hiyo ya kisheria, wengine wameanza wizi wa reja reja baadae utakuwa wizi wa kudumu, sasa ili kuwakomesha hawa ni lazima tuanze kufunga wawili watatu kama ninyi wenyewe mlivyopendekeza hapa,” Alisema.

Hadi kufikia tarehe 23.04.2020 halmashauri za Mkoa wa Rukwa zinadai zaidi ya shilingi milioni 928 za makusanyo ambayo hayajawasilishwa benki kutoka kwa watendaji, huku halmashauri ya Wilaya ya kalambo ikiwa ya pili kwa kudai ambapo watendaji wake wanadaiwa shilingi 260,496,059 na madiwani wa halmashauri hiyo wakidai zaidi ya shilingi milioni 80.

No comments:

Post a Comment

Pages