Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi Sichon
Baadhi ya
Madiwani waliohudhuria Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kilichohusu
utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo.
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Baraza
la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Daudi Sichone
ametangaza kuwafukuza kazi pamoja na kuwapeleka mahakamani watendaji wa vijiji
wanaokusanya mapato na kutowasilisha mapato hayo benki kwaajili ya utekelezaji
wa matumizi mbalimbali ya halmashauri hiyo.
Amesema kuwa tabia
hiyo ilianza kwa watendaji wachache kutumia fedha wanazokusanya hali
iliyopelekea na watendaji wengine kuiga tabia hiyo na matokeo yake kuwa desturi
kwa watendaji hao kutumia fedha za makusanyo huku ikisomeka kuwa ni wadaiwa
(defaulters) jambo ambalo Mwenyekiti huyo analipinga na kusema watendaji hao
sio wadaiwa bali ni wezi wa fedha za halmashauri na hivyo wachukuliwe hatua
kama wezi.
“Imekuwa Shida, kuna
watendaji ambao sasa hivi wanaona kuwa TAKUKURU nako ni kama nyumbani, na sisi
njia nyingine ambayo tunayo, nguvu yetu tuliyonayo ni ya kuwafukuza tu na
kuwapeleka mahakamani, kwasababu hatuna namna, tumewapeleka kwenye vyombo
ambavyo ndio tunavitegemea, zimefanya kazi yake kwa nguvu zote, tumekwenda
hivyo lakini…” Alisema.
Aliongeza kuwa kuna
baadhi ya watendaji wadaiwa ambao wameshajiandikisha ofisi ya Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kalambo ili ifikapo tarehe 30.05.2020 wawe
wamemaliza kulipa fedha hizo na kushauri kuwa watendaji hao wasisubiriwe hadi
ifike tarehe hiyo, kwani kuna watendaji ambao madeni yao ni makubwa na hivyo
hawataweza kulipa fedha hizo kwa pamoja na kuitaka ofisi hiyo kuweka utaratibu
wa watendaji hao kulipa kidogokigdogo.
Maamuzi hayo
yalifikiwa na Mwenyekiti huyo baada ya kukubaliana katika vikao vya kamati ya
fedha, Uongozi na Mipango jambo ambalo liliungwa mkono na waheshimiwa madiwani wote
waliohudhuria katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo tarehe
2.5.2020 kilichohusu utekelezaji wa hoja za ukaguzi na mapendekezo ya mdhibiti
na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini.
Awali akichangia hoja
ya kuchukuliwa hatua za kufukuzwa watendaji hao, Diwani wa kata ya Mambwenkoswe, Edwin Msipi alisema kuwa halmashauri hivi sasa inasota kutokana na fedha
nyingi kuwemo katika mifuko ya watendaji na hivyo kupelekea miradi mingi ya
halmashauri kushindwa kutekelezeka na hivyo kulitaka baraza hilo kuwa na mkakati
wa kuwashughulikia watendaji hao.
“Kwakweli tuna-suffer
kwenye halmashauri hii, kama halmashauri zote za Tanzania ziko hivi sijui, ila
tunasota na pesa zipo kwa watu ambao walipoanza kuiba kidogo kidogo ikawa ni
fundisho hata kwa wengine sasa, kwamba aah, sisi kule si tunadaiwa tu,
tutapeleka nusu nusu, mkakati haujafanyika isipokuwa tukizungumza kwenye chemba
kama hivi, tunazungumza lakini yataishia hapa hapa,” Alisisitiza.
Katika maelezo yake
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ambaye ni mwalikwa wa kikao hicho
alisema kuwa jukumu la kwanza la madiwani ni kusimamia ukusanyaji wa mapato ya
halmashauri na kuongeza kuwa hao wadaiwa (defaulters) ni wa kwao na wapo ndani
ya uwezo wao na kuwathibitishia kuwa endapo watahitaji msaada wa serikali, ofisi
yake na ofisi ya mkuu wa Wilaya zipo tayari kutoa msaada huo.
“Kwahiyo tunataka kwa
mkoa mzima milioni 450 ziwe zimeshakusanywa na kulipwa waheshimiwa madiwani,
kufikia mwisho wa mwezi huu, kwahiyo ni lazima tupambane kufa na kupona na hawa
‘defaulters’, sio tu kuwafunga lakini kwanza wairudishe hiyo hela ili tupate hela
ya kuwalipa madiwani, halafu hatua nyingine itafuata hiyo ya kisheria, wengine
wameanza wizi wa reja reja baadae utakuwa wizi wa kudumu, sasa ili kuwakomesha hawa
ni lazima tuanze kufunga wawili watatu kama ninyi wenyewe mlivyopendekeza
hapa,” Alisema.
Hadi kufikia tarehe
23.04.2020 halmashauri za Mkoa wa Rukwa zinadai zaidi ya shilingi milioni 928 za
makusanyo ambayo hayajawasilishwa benki kutoka kwa watendaji, huku halmashauri
ya Wilaya ya kalambo ikiwa ya pili kwa kudai ambapo watendaji wake wanadaiwa
shilingi 260,496,059 na madiwani wa halmashauri hiyo wakidai zaidi ya shilingi
milioni 80.
No comments:
Post a Comment