May 13, 2020

KATA YA KITWIRU YAKITHIRI KWA VITENDO VYA UPORAJI NA UKABAJI


Diwani wa Kata ya Kitwiru Baraka Kimata akiongea na wananchi jinsi ya kupambana na vitendo vya ukabaji na uporaji wa mali unaofanywa na vibaka katika mtaa wa Nyamuhanga. (Picha na Maktaba).


Na Fredy Mgunda, Iringa

Wananchi wa kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa wameiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuanzisha mkakati maalum utakaowashirikisha wakazi wa maeneo hayo ili kudhibiti ongezeko la vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo matumizi ya mihadarati aina ya bangi pamoja na ukabaji na uporaji wa mali hasa nyakati za usiku.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa mtaa wa Nyamuhanga katani humo walisema kuwa vitendo vya ukabaji na uporaji wa mali za wananchi vimekithiri kiasi kwamba vinatishia maisha ya wakazi wa mtaa huo na kusababisha miongoni mwao kushindwa kufanya shughuli zao kwa uhuru kama ilivyo katika maeneo menginine ya Manispaa hiyo.

Walisema kuwa kwa sasa kumezuka kundi la vijana wanaotumia bodaboda kwa ajili ya uporaji wa wananchi wanaoshukia katika kituo cha daladala cha Ivory nyakati za usiku kutokana na maeneo hayo na mengineyo katika mitaa ya Nyamuhanga kuwa na vichaka na mapori yanayotumiwa na wahhalifu kama maficho wakati wakijipanga kutenda uhalifu huo

Wananchi hao waliongeza kuwa wanaofanya vitendo vya ukabaji na uporaji wengi wao ni vijana ambao wamekuwa wanatumia madawa ya kulevya aina ya bangi na inayowapelekea kufanya vitendo hivyo vya kiharifu ambavyo vinaleta madhara makubwa kwa usalama na uchumi wa wananchi.

Walisema wamekuwa wanatoa taarifa mara kwa mara kwa uongozi wa serikali ya mtaa,Diwani na Jeshi la Polisi ili kushughulikia tatizo hilo ambalo limekuwa kero kwa wananchi lakini hakuna matokeo ya moja kwa moja ya kuthibiti vitendo hivyo vya ukabaji na uporaji.

“Tumelalamika sana kuhusiana na janga hili la ukabaji na uboraji kwa kuwa limekuwa limedumu kwa muda mrefu bila kutafutiwa ufumbuzi wa moja kwa moja” Walisema

Miongoni mwa wananchi hao waliishauri Seriakali za mitaa ya kata ya Kitwiru kuanzisha vikundi vya ulinzi shirkishi baina ya wananchi na Jeshi la polisi ili ikiwezekana ipigwe kura ya siri kuwataja wahalifu wanaoshukiwa kutenda uhalifu huo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kukomesha vitendo hivyo.

Wakazi wa eneo hilo sanjari na hayo walishauri kuanzishwa kwa utaratibu wa ulinzi wa kujitolea kupitia sungusungu ili kuwe na doria za mara kwa mara nyakati za usiku.

kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kitwiru Baraka Kimata akizungumzia kuhusu vitendo hivyo vya uhalifu alikiri kukithiri kwa vitendo hivyo na kueleza kuwa kinachochangia hali hiyo ni mazingira ya mapori na vichaka vilivyopo hasa katika mitaa ya nyamuhanga kwani wakazi walio wengi katika maeneo hayo wamelima mahindi katika maeneo ya pembezoni mwa barabara na kusababisha wahalifu kujificha.

Kimata alisema kuwa pamoja na jitihada wanazochukua ikiwemo kuanzisha Sungusungu katika baadhi ya mitaa, kushirikiana na jeshi la polisi na viongozi wa serikali za mitaa kwa ajili ya doria na kuwafichua wahalifu lakini bado mbinu hizo zimeshindwa kufikia mafanikio ya kutosha.

Hata hivyo diwani huyo aliitaja sababu nyingine ni kata hiyo kuwa na eneo kubwa la kiutawala ikiwa na zaidi ya wakazi 15 Elfu wote hao wakitegemea  askari katika kituo kimoja cha polisi hivyo kutokuwapo kwa uwiano sawa wakati wa kushughulikia changamoto za kiuhali huku pia akiwataka wamiliki wa viwanda katika eneo hilo kuweka taa zitakazomulika maeneo ya barabara na uzio unaotumiwa na baadhi ya watu kutekeleza uhalifu huo.


No comments:

Post a Comment

Pages