Diwani wa Kata ya Kitwiru Baraka Kimata akiongea na wananchi jinsi ya kupambana na vitendo vya ukabaji na uporaji wa mali unaofanywa na vibaka katika mtaa wa Nyamuhanga. (Picha na Maktaba).
Na Fredy Mgunda, Iringa
Wananchi wa kata ya Kitwiru
Manispaa ya Iringa wameiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na
usalama kuanzisha mkakati maalum utakaowashirikisha wakazi wa maeneo hayo ili kudhibiti
ongezeko la vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo matumizi ya
mihadarati aina ya bangi pamoja na ukabaji na uporaji wa mali hasa nyakati za
usiku.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti baadhi ya wananchi wa mtaa wa Nyamuhanga katani humo walisema kuwa
vitendo vya ukabaji na uporaji wa mali za wananchi vimekithiri kiasi kwamba vinatishia
maisha ya wakazi wa mtaa huo na kusababisha miongoni mwao kushindwa kufanya
shughuli zao kwa uhuru kama ilivyo katika maeneo menginine ya Manispaa hiyo.
Walisema kuwa kwa sasa kumezuka
kundi la vijana wanaotumia bodaboda kwa ajili ya uporaji wa wananchi wanaoshukia
katika kituo cha daladala cha Ivory nyakati za usiku kutokana na maeneo hayo na
mengineyo katika mitaa ya Nyamuhanga kuwa na vichaka na mapori yanayotumiwa na
wahhalifu kama maficho wakati wakijipanga kutenda uhalifu huo
Wananchi hao waliongeza kuwa
wanaofanya vitendo vya ukabaji na uporaji wengi wao ni vijana ambao wamekuwa
wanatumia madawa ya kulevya aina ya bangi na inayowapelekea kufanya vitendo
hivyo vya kiharifu ambavyo vinaleta madhara makubwa kwa usalama na uchumi wa wananchi.
Walisema wamekuwa wanatoa
taarifa mara kwa mara kwa uongozi wa serikali ya mtaa,Diwani na Jeshi la Polisi
ili kushughulikia tatizo hilo ambalo limekuwa kero kwa wananchi lakini hakuna
matokeo ya moja kwa moja ya kuthibiti vitendo hivyo vya ukabaji na uporaji.
“Tumelalamika sana kuhusiana na
janga hili la ukabaji na uboraji kwa kuwa limekuwa limedumu kwa muda mrefu bila
kutafutiwa ufumbuzi wa moja kwa moja” Walisema
Miongoni mwa wananchi hao waliishauri
Seriakali za mitaa ya kata ya Kitwiru kuanzisha vikundi vya ulinzi shirkishi
baina ya wananchi na Jeshi la polisi ili ikiwezekana ipigwe kura ya siri
kuwataja wahalifu wanaoshukiwa kutenda uhalifu huo ili waweze kuchukuliwa hatua
za kisheria kukomesha vitendo hivyo.
Wakazi wa eneo hilo sanjari na
hayo walishauri kuanzishwa kwa utaratibu wa ulinzi wa kujitolea kupitia
sungusungu ili kuwe na doria za mara kwa mara nyakati za usiku.
kwa upande wake Diwani wa Kata
ya Kitwiru Baraka Kimata akizungumzia kuhusu vitendo hivyo vya uhalifu alikiri
kukithiri kwa vitendo hivyo na kueleza kuwa kinachochangia hali hiyo ni
mazingira ya mapori na vichaka vilivyopo hasa katika mitaa ya nyamuhanga kwani
wakazi walio wengi katika maeneo hayo wamelima mahindi katika maeneo ya
pembezoni mwa barabara na kusababisha wahalifu kujificha.
Kimata alisema kuwa pamoja na
jitihada wanazochukua ikiwemo kuanzisha Sungusungu katika baadhi ya mitaa,
kushirikiana na jeshi la polisi na viongozi wa serikali za mitaa kwa ajili ya
doria na kuwafichua wahalifu lakini bado mbinu hizo zimeshindwa kufikia
mafanikio ya kutosha.
Hata hivyo diwani huyo aliitaja
sababu nyingine ni kata hiyo kuwa na eneo kubwa la kiutawala ikiwa na zaidi ya
wakazi 15 Elfu wote hao wakitegemea
askari katika kituo kimoja cha polisi hivyo kutokuwapo kwa uwiano sawa
wakati wa kushughulikia changamoto za kiuhali huku pia akiwataka wamiliki wa
viwanda katika eneo hilo kuweka taa zitakazomulika maeneo ya barabara na uzio
unaotumiwa na baadhi ya watu kutekeleza uhalifu huo.
No comments:
Post a Comment