HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 26, 2020

Wajane watakiwa kutokata tamaa

Na Janeth Jovin

DIWANI wa Kata ya Ukonga Juma Mwipopo (Chadema) amewataka wajane kutokata tamaa licha ya kupitia changamoto mbalimbali katika kutunza na kulea familia zao kutokana na kuondokewa na wapendwa wao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi wakati wa kuadhimisha siku ya wajane duniani, Mwipopo alisema anatambua kuwa wajane wakakumbana na changamoto nyingi lakini ni muhimu kutokata tamaa na kuhakikisha wanjishughulisha na ujasiriamali ili kuweza kumudu kulea familia zao.

Alisema kutokana na kundi hilo kukabiliwa na changamoto nyingi anaiomba Serikali kulipatia msaada utakaowawezesha kujikwamua na kubadilisha maisha yao kwa kuwaingia katika makundi yanayopaswa kupata mikopo ya halmashauri.

“Tunaiomba Serikali ili kundi la wajane lijitegemee katika upewaji wa mikopo pia waondolewe masharti magumu katika mkopo huo wa halmashauri maana sasa hivi ili wakopesheke lazima wawe na hati ya nyumba ambapo wengine wanaishi katika nyumba za kupanga.

Ni wakati sasa Serikali inapaswa kuweka mpango utakaohakikisha kila mtaa kundi hili linafunguliwa mradi wa pamoja ili waweze kuondokana na unyonge na hatimaye waweze kuzisaidia familia zao,” alisema.

Alisema ni muhimu pia Serikali ikaangalia upya jinsi ya kuwasaidia wajane wasiojiweza kupata kadi za matibabu bure na watoto wao ili kuwapunguzia mzigo walio nao katika kulea familia.

“Tunawaomba wajane wote kwa kuwa unaelekea katika uchaguzi mkuu, basi Chadema kanda ya Pwani tunawakaribisha kugombea katika nafasi mbalimbali ndani ya chama ili mkichaguliwa mpate fursa ya kutetea wenzenu na maslahi yenu badala ya kutegemea kuongelewa,” alisema

No comments:

Post a Comment

Pages