July 07, 2020

Bodi ya mikopo yafanikiwa kukusanya Bilioni 192 kutoka kwa wakopaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ((HESLB), Abdul Razaq Badru.


 Na Janeth Jovin

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema, hadi kufikia Juni mwaka huu, imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi billioni 192 kutoka kwa wakopaji wa bodi hiyo.


Hayo yamebainishwa jana  na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdul Razaq Badru wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu ‘Sabasaba’ , yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Badru amesema, makusanyo ya mikopo hiyo iliyokusanya ni kutoka kwa wakopaji wa mikopo katika bodi hiyo.

Amesema, mwaka 2015 hadi Juni 2020 jumla ya shilingi trilioni 2.6 zimewekezwa kwenye utoaji mikopo kwa wanafunzi, ambayo ni uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu.

“Bodi imewekeza sana kwenye utoaji mikopo na jinsi wanavyorejesha ndivyo tunavyoongeza wakopaji wengi, tunataka wanufaika waongezeke na kila mwenye kufaulu asikose kusoma hasa wale wa familia masikini ambao ndio kipaumbele chetu,”amesema Badru.

Hata hivyo amesema, kwa mwaka huu mpya wa masomo wamejipanga kufika kila mkoa kusaidia wanafunzi jinsi ya kujaza fomu za kuomba mikopo ili kupunguza makosa yanayofanywa na baadhi yao yanayosababisha wengine kukosa mikopo.

Badru amesema, bodi hiyo inatarajia kufungua dirisha la kuomba mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 Julai 20 mwaka huu.

Amesema, wameamua kutangaza mapema maandalizi ya kufungua dirisha hilo ili kuwapa muda waombaji kujiandaa ili matokeo ya mitihani yao ya kuhitimu masomo yatokapotoka waombe nafasi za kujiunga na vyuo mbalimbali.

Alibainisha kuwa, mwaka huu wa masomo 2020/2021 serikali imeidhinisha jumla ya sh Bilioni 468, kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 125,000 wanaosoma wakiwemo wapya 50,000 wanaotarajiwa kupata mkopo mwaka mpya wa masomo.

“Tumekuja sabasaba kuwaambia wazazi na wanafunzi kwamba tupo na dirisha kwa ajili ya kuomba mikopo kwa mwaka mpya wa masomo 2020/2021 tutafungua Julai 20 mwaka huu, amesema Badru.

Amesema, kila mwaka bajeti ya mikopo huongezeka ambapo mwaka jana ilikuwa Sh bilioni 450 na mwaka huu imeongezeka kwa bilioni 18 .

Kuhusu maonesho amesema “Sisi Maonesho haya yanatusaidia sana kwa sababu huwa ni maandalizi ya kuanza msimu mpya na tuko tayari kufungua msimu huo kwa mwaka wa masomo 2020/21, bajeti mpya ya serikali iliyopitishwa bungeni ya Bilioni 468 hii itatuwezesha kulipia wanafunzi wapya wasiopungua 50,000”, amesema Badru

alibainisha kuwa kwa mwaka huu wa masomo unaoanza novemba kutakuwa na wanafunzi wapya wanaofaidika na mkopo wa elimu ya juu wapatao 50, 000 na kufanya idadi ya wanafunzi wanaolipiwa na Bodi hiyo kuwa 225,000 ambapo wote watakuwa wanafaidika na bajeti mpya ya bilioni 468.

No comments:

Post a Comment

Pages